Kimataifa

Kurudisha raslimali ya Afrika iliyoibwa

February 15th, 2020 2 min read

Na KEN WALIBORA

MUUNGANO wa Afrika (AU) umetangaza mapambano dhidi ya upitishaji haramu wa fedha na kuimarisha urejeshaji wa mali ya Afrika iliyoporwa.

Tangazo hilo limetolewa baada ya pendekezo la serikali ya Nigeria kuutaka Muungano huo kuzidisha juhudi za kurudisha raslimali za Afrika zilizoporwa na kurundikwa nje ya bara na watu binafsi na mashirika kwa kutumia njia zisizo halali.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa mnamo Februari 10, 2020, kwenye jiji kuu la Ethiopia, Addis Ababa, Shirika la Muungano wa Usemezakano kuhusu Afrika (CoDA) limedai kwamba Mkakati wa Pamoja wa kurejesha raslimali za Afrika, ni wenzo muhimu katika kuliwezesha bara hili kupata tena raslimali zake zilizoibwa na kupatikana kwa upitishaji haramu wa fedha.

Mali nyingi za Afrika zilizoibwa zinapatikana kwenye nchi za nje.

Shirika la CoDA limekuwa jukwaa mwafaka la kujadili kwa uwazi masuala yanayohusu bara la Afrika, nalo linashirikiana na watunga sera na wadau kumulikia maswala kama vile usalama, amani, utawala na maendeleo.

Mapambano ya pamoja dhidi ya upitishaji haramu fedha barani Afrika yameibuka wakati uporaji wa raslimali za Afrika kwa hila za viongozi wa Kiafrika na washirika wao wa kimataifa.

Katibu mtendaji wa CoDA, Souad Aden-Ousman, alisema kwamba ulanguzi wa fedha za Afrika husababisha kusuasua kwa usalama, uchumi na kutoafikiwa kwa malengo ya maendeleo endelevu.

Ousman anasema ulanguzi wa fedha katika nchi moja huathiri nchi jirani.

Alitoa mfano wa Somalia na Sudan Kusini ambapo kuna ulanguzi mkubwa wa fedha ambao huvuka mipaka na kuingia katika nchi jirani.

Alisema nchi jirani za Somalia na Sudan Kusini zimegeuzwa kuwa vituo vya uwekezaji wa waporaji wa hazina za Somalia na Sudan Kusini. Hali hii ni tishio kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi hizo.

Kuwezesha ulanguzi wa fedha kumechangia kutatiza mifumo ya kimatafa ya fedha na kudumaza maendeleo ya asasi za Afrika.

Tafiti zinaonesha kwamba Afrika imepoteza zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 50 kwa ulanguzi wa fedha. Aliyekuwa kiongozi wa Libya Muamar Gaddafi alihamisha zaidi ya dola bilioni 16 za Marekani fedha za umma naye aliyekuwa Rais wa Gambia Yahya Jammeh, zaidi ya dola bilioni moja.

Miongoni mwa wababe wengine waliozitwaa raslimali za Afrika walipokuwa mamlakani ni pamoja na Mobutu Seseko wa Zaire (ambayo sasa ni Jamhuri ys Kidemokrasia ya Kongo) na Siad Barre wa Somalia.

Sasa linalosubiriwa na utekelezaji wa tamko la kukomesha ulanguzi wa fedha barani Afrika.