Habari Mseto

KURUNZI YA PWANI: Bunge la Kilifi laidhinisha hoja kufuta vibarua 1,000

March 22nd, 2019 2 min read

Na CHARLES LWANGA

WAFANYAKAZI takriban 1,000 walioajiriwa kama vibarua huenda wakapoteza ajira baada ya Bunge la Kaunti ya Kilifi kuidhinisha hoja ya kuwafuta kazi.

Wafanyakazi hao wako chini ya Bodi ya Kuajiri Wafanyakazi Kaunti (CPSB).

Hatua hiyo imeibua hofu kuu kwa wanaotegemea kazi hizo huku baadhi ya wakazi wakiingia kwa mitandao ya kijamii kuikashifu.

Hoja hiyo ambayo iliwasilishwa na diwani wa Kayafungo, Bw Alphonce Mwayaa, inasimamisha kazi watu wote wanaofanya vibarua chini ya bodi hiyo, isipokuwa wale wanaohudumu hospitalini.

Katika hoja hiyo, Bw Mwayaa analenga kuwafuta wafanyakazi wote waliondikwa na maafisa wakuu wa serikali ya kaunti kufanya kazi za mkataba bila idhini ya bodi ya CPSB.

Akizungumza na Taifa Leo kwa simu, Bw Mwayaa alisema lengo la hoja hiyo ni kuhakikisha kuwa sheria imefuatwa kikamilifu ili kuleta uwazi katika huduma serikalini na jinsi ya kupata ajira.

“Tunataka kuhakikisha kuwa mambo ya kuandikwa kazi kwa sababu mtu ni shangazi au mjomba au ana uhusiano wa kijamii au urafiki na maafisa wakuu serikalini inatupwa katika kaburi la sahau,” alisema.

Aliongeza,“Wakishafutwa, wakazi watawasilisha maombi ya kazi upya na kuajiriwa kulingana na stakabadhi zao.”

Wakati huo huo, Bw Mwayaa alisema hoja hiyo pia inanuia kupunguza gharama inayotumika kulipa mishahara kwani huenda baadhi ya fedha hutumika kulipa wafanyakazi hewa.

“Kwa mfano, katika idara ya maji pekee imekuwa na takriban wafanyakazi 478 wanaofanya vibarua na kusababisha gharama ya mishahara ya Sh17 milioni kwa kipindi cha miezi minne pekee,” alisema.

Lakini baadhi ya madiwani ambao hawakutaka kutajwa walidai kuwa hoja hiyo ilitokana na msukumo wa kisiasa baina ya madiwani ambao wanataka kuwaajiri ‘watu wao’.

“Baadhi ya madiwani wamekuwa wakitaka kuwaajiri watu wao lakini wamekuwa wakishindwa kwa sababu nafasi hizo zimemilikiwa na wafanyakazi waliowekwa na wapinzani wao katika serikali iliyopita,” alisema.

Wakati huo huo, diwani wa Sokoni, Gilbert Peru, ambaye alikosa kuhudhuria kikao hicho cha bunge, alimkashifu diwani mwenzake kwa kuwasilisha hoja hiyo akisema kuwa anawagandamiza vijana wanaopambana kupata ajira.

“Wakati sisi viongozi vijana tunalalamika kuwa fedha zinazotengewa idara ya vijana ni kidogo na zinafaa kuongezwa, wewe unajishughulisha na kuwasilisha hoja wa kuhatarisha vijana. Nia yako kwa masuala ya vijana si nzuri hata kidogo,” alisema.

Kutatua mzozo

Hata hivyo, Karani wa Kaunti hiyo, Bw Anorld Mkare, aliambia Taifa Leo kuwa watahakikisha wametatua mzozo huo kwa njia ya haki na utaratibu unaostahili ili kuhakikisha hakuna yeyote atakayedhulumiwa.

Mnamo Jumanne kaunti ya Mombasa pia ilionekana kwenda kinyume na matarajio ya Gavana Ali Hassan Joho, ilipoidhinisha hoja ya kumtimua waziri wake wa barabara na miundomsingi, Tawfiq Balala, wakidai hajamakinika na pia utendaji kazi duni
Gavana Joho aliomba utulivu miongoni mwa wakazi na kuhimiza ripoti kuhusiana na hatua hiyo iwe ya haki bila mapendeleo yoyote.