Makala

KURUNZI YA PWANI: EACC yachunguza ubaguzi katika ugavi wa basari Kibarani

November 13th, 2018 3 min read

NA SAMUEL BAYA

Tume ya kupambana na ufisadi (EACC) eneo la Pwani imeanzisha uchunguzi kuhusu ugawaji duni wa basari katika kamati ya basari ya wadi ya Kibarani, Kaunti ya Kilifi.

Kamati hiyo imekumbwa na madai ya ubaguzi katika ugawaji wa basari na tayari hazina ya basari katika kaunti ya Kilifi ilikuwa imeisimamisha kazi kamati hiyo mwezi uliopita.

Kumekuwa na madai kutoka kwa wakazi kuwa bodi hiyo iko na upendeleo katika kugawa fedha za masomo.

Ingawa lengo la basari ni kuwasaidia wanafunzi werevu kutoka jamii maskini kuendelea na masomo, kamati hiyo imelaumiwa kwa kuwanufaisha washirika wa karibu wa wanakamati.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo afisini mwake, mwenyekiti wa hazina hiyo Bw Mulewa Katana alisema waliarifiwa na EACC kwamba tume ilikuwa ikichunguza kamati hiyo hivyo ilikuwa ni makosa kuivunja. Na Samuel Baya

“Ni kweli tulikuwa tumesimamisha bodi hiyo baada ya lalama nyingi kutoka kwa wananchi. Wakazi wengi walikuwa wakilalama kuhusu jinsi wasimamizi wa kamati hiyo wamekuwa wakijitengea fedha nyingi kwa washirika wao na jamii zao.

Baada ya sisi kama hazina kuisimamisha kamati hiyo, mmoja wao aliamua kulipeleka suala hilo kwa tume ya kukabiliana na ufisadi. Tume hiyo baadaye ilituandikia barua kutuarifu kwamba wanafanya uchunguzi,” akasema Bw Mulewa.

Alisema kupitia kwa ushauri wa EACC hazina hiyo ilibatili uamuzi wake ili kutoa fursa kwa tume hiyo kuendelea na uchunguzi wake.

Bw Mulewa alisema hayo huku katibu wa kaunti hiyo Bw Arnold Mkare akiwaonya maafisa wasimamizi wa wadi kwamba watachukuliwa hatua kali endapo itabainika wanahusika na ubadhirifu wa fedha hizo za basari.

“Fedha za basari ni za umma na wala sio pesa za mtu binafsi. Tumepata habari kwamba kuna baadhi ya wasimamizi wa wadi wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya kamati za basari za wadi kufanya ufisadi na upendeleo. Hili ni onyo kwamba hatutavumilia tena, ” akaonya Bw Mkare.

Hazina hiyo ya basari hutenga kiasi cha Sh350 millioni kila mwaka ili kugharamia masomo kwa wanafunzi ambao hawana uwezo wa kulipa karo.

Katika wadi 35 za kaunti hiyo, kila wadi hupokea kiasi cha Sh10 millioni kila mwaka kwa ajili ya kuwapa karo wanafunzi.

Tahadhari ya ufujaji na ugawaji mbaya wa fedha hizo ulianza mwezi uliopita pale mwakilishi wa wadi hiyo Bw John Mwamutsi alipomuandikia barua hazina hiyo baada ya madai kuibuka.

Katika barua hiyo ya Oktoba 26, Bw Mwamutsi aliandika akiomba kamati hiyo isimamishwe haraka na uchunguzi uanzishwe.

“Kumeibuka madai mabaya sana ya usambzaji wa fedha za kamati ya basari ya Kibarani. Tafadhali kama hazina, tunaomba muisimamishwe kamati hiyo na kuruhusu uchunguzi ufanyike,” ikasema barau hiyo ambayo Taifa Leo ilifanikiwa kupata nakala yake.

Naye Bw Mulewa katika barua yake ya Oktoba 27 alitangaza kusimamishwa kwa kamati hiyo hadi pale uchunguzi ufanyike na kupata tatizo ambalo linakumba kamati hiyo.

“Kupitia narua ambayo tulipata kutoka kwa mwakilishi wa wadi ya Kibarani ninakufahamisha kwamba kamati yako imesimamishwa kuendelea na shughuli zozote hadi uchunguzi kamili utakapofanyika.

Kwa sasa ninamruhusu mwakilsihi wa wadiu kuanzisha juhudi za kuweka kamati ya muda ili kuhakikisha kwamba kumebuniwa kamati ya muda ndani ya wiki mbili zijazo,” akasema Bw Mulewa.

Hata hivyo mnamo Oktoba 29, hazina hiyo ilipata barua kutoka kwa tume ya kupambana na ufisadi ikiitaka hazina hiyo iachane na mpango wa kusimamisha kamati hiyo.

‘Tume ya kupambana na ufisadi inachunguza utumiaji mbaya wa fedha za umma katika kamati ya basari ya Kibarani kama jambo hilo lilivyoripotiwa kwetu.

Tayari jambo hili lilikuwa limewasilishwa kwako awali kulingana na barua ambayo tuko nayo. Tuko na habari kwamba mwenyekiti wa sasa wa kamati hiyo alirekodi taarifa na afisi yetu na uchuguzi unaendelea.

Haukufaa kuivunja kamati hiyo kwa sababu uchunguzi unaendelea,” ikasema sehemu ya barua hiyo ya EACC.

Naye Bw Mulewa katika barua ya Oktoba 31, aliandikia tume hiyo ya EACC akigeuza barua ya awali ya kuivunja kamati hiyo.

“Tumeona yale ambayo mulisema katika barua yenu na yote tumeyasikia na kwa sababu hiyo hazina ya fedha za basari ya Kilifi imebatilisha uamuzi wa kuivunja kamati hiyo ya Kibarani ili kuruhusu uchunguzi uendelee,” ikasema sehemu ya barua hiyo.

Tangu ianzishwe, hazina hiyo imesaidia jumla ya wanafunzi 220,416 kuendelea na masomo yao. Idadi kubwa kati ya hawa ni wale ambao wanasomea katika shule za sekondari ambao kufikia sasa ni 157,758.