Makala

KURUNZI YA PWANI: Kampeni ya kuangamiza unywaji wa pombe haramu yaanza

August 6th, 2018 2 min read

Na HAMISI NGOWA

VIONGOZI wa kidini pamoja na mashirika ya kijamii kwa ushirikiano na maafisa wa utawala katika eneobunge la Likoni Kaunti ya Mombasa sasa wameanzisha mbinu mpya za kukabiliana na unywaji pombe haramu na utumizi wa dawa za kulevya miongoni mwa vijana katika eneo hilo.

Mbinu hizo mpya ambazo wakazi wana imani kwamba zitasaidia kuangamiza ulevi wa pombe pamoja na utumizi wa bangi miongoni mwa vijana wa eneo hilo ni operesheni za ghafla za kuwanasa wauzaji na wagema wa pombe hizo.

Mwishoni mwa wiki, viongozi hao walizindua rasmi operesheni hiyo iliyopewa jina ‘maliza pombe haramu na bangi mitaani’ ambapo watu watatu walimakatwa pamoja na zaidi ya lita 200 za Chang’aa.

Viongozi hao aidha waliharibu kwa kuviteketeza kwa moto baadhi ya vifaa vilivyonaswa wakati wa operesheni hiyo ambavyo vinadaiwa kutumika katika shughuli za biashara hiyo.

Naibu Kamishna wa eneo hilo Bw Erick wa Mlevu ambaye aliongoza opereresheni hiyo,alithibitisha kukamatwa kwa washukiwa hao huku akiwaonya maafisa wa polisi dhidi ya kuwaalichia kwa njia zisizoeleweka.

Bw Wamlevu alisema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya afisa yeyote wa serikali katika eneo hilo atakayepatikana akijihusisha kwa njia yoyote ile ya kujaribu kuwahifadhi wauzaji pombe haramu, bangi pamoja na dawa za kulevya.

“Nataka kuwaambia kwamba mkiona afisa yoyote wa serikali akichukuwa bahasha kwa hawa watu wanaoangamiza vijana wenu kwa kuwauzia vileo, tafadhalini tumieni simu zenu kuwapiga picha na mniletee ili niwe na ushahidi wa kutosha wa kuwaadhibu,’’ akasema.

Walemavu aidha aliwashukuru viongozi hao kwa kujitolea na kuahidi kwamba serikali itaendelea kushirikiana nao katika vita hivyo kwa lengo la kuwanusuru vijana.

Alidokeza kwamba operesheni hiyo itakuwa ikifanyika kila wiki hadi maskani zote zinazotumiwa kwa shughuli hiyo haramu zitakapoangamizwa.

Naye mwenyekiti wa Baraza la walimu wa kiislamu eneo hilo Ustadhi Suleiman Kilembi alisema japo opereresheni hiyo ilianza dhidi ya wauzaji wa pombe haramu,pia itawaandama na wale wanaouza bangi na dawa za kulevya. Aliihimiza jamii kuunga mkono juhudi za viongozi hao ili kuhakikisha wanaojihusisha na biashara hiyo wanakamatwa na kukumbana na mkono wa sheria.

“Sisi kama viongozi wa kidini tumesema imetosha na kwamba sasa hatutakaa kimya tukiangalia watu wachache wakiangamiza vizazi vyetu.Tutawasaka popote walipo hadi tuwaondoe,’’ akasisitiza.

Lakini kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirika la Coast People Struggle For Human Rights, Bw Hamisi Mifale aliitaka serikali kutowapa msamaha wala dhamana watu wanaotuhumiwa kwa ulanguzi wa mihadarati.

Alisema hukumu kali zinafaa kuwekwa kwa wanaopatikana na hatia ya ulanguzi wa dawa za kulevya ikiwemo kifungo cha maisha gerezani ili kuwa mfano kwa wengine.

Alisema miaka mitatu iliyopita,wakazi wa eneo hilo walianzisha vita vikali dhidi ya walanguzi wa dawa za kulevya lakini juhudi hizo zikalemazwa na hatua ya kupewa msamaha kwa baadhi ya washukiwa wakuu wa ulanguzi wa dawa za kulevya eneo hilo.

“Changamoto kubwa ilioko ni sheria na hukumu ndogo inayopewa walanguzi wa dawa za kulevya, nadhani kuna haja kwa wabunge kuipiga msasa ili wanaopatikana na hatia ya ulanguzi wa mihadarati wawe wanapewa hukumu kali zaidi,’’ akasema.