Makala

KURUNZI YA PWANI: Kiini cha vifo vingi vya kina mama wajawazito Pwani

June 18th, 2018 4 min read

Na WINNIE ATIENO

Utafiti wa afya wa mwaka wa 2014 Kenya Demographic Health Survey unaonyesha kuwa kati ya wanawake 5,000 hadi 6,000 wajawazito huaga dunia wanapojifungua humu nchini huku watoto wachanga 22 kati ya 1,000 hufariki wanapozaliwa.

Kaunti za Tana River, Lamu, Kilifi na Kwale miongoni mwa kaunti eneo la Pwani ambapo kuna visa vingi vya kina mama wajawazito kuaga.

Mapema mwaka huu, Subira Hamisi alikuwa na furaha akisubiri kujifungua mtoto wake wa pili.

Lakini mambo yalibadilika mwezi wa Mei tarehe mbili wakati mama huyo aliyekuwa na ujauzito wa miezi tisa kuanza kusikia maumivu ya ujauzito alipokuwa akilala nje ya nyumba yao huko Gombato eneo la Ukunda kaunti ya Kwale.

Aliamua kustahimili maumivu hayo hadi kesho yake Mei tarehe 3, siku ambayo alitakiwa kwenda kliniki ya kina mama wajawazito hapo Gombato.

“Alikuwa na maumivu chini ya tumbo na chini ya maziwa yake. Mwanangu alikuwa ajifungue wakati wowote mwezi huo. Hatukukuwa na wasiwasi wowote sababu alikuwa anatarajiwa kwenda kwenye kliniki yake hapo kituo cha afya cha Gombato ambayo iko mita 200 kutoka hapa kwetu yumbani,” akasema mamake Bi Hamisi, Mwanaasha Omar.

Alipoenda katika hospitali hiyo, Bi Hamisi alidhani atalazwa ili ajifungue lakini mhudumu wa afya alimhudumia na akamruhusu kwenda nyumbani.

“Tulishangaa sana kwa nini hakulazwa ilhali alikuwa na maumivu na isitoshe muda wake wa kujifungua ulikuwa umewadia. Nikaamua kumwangalia kwa makini sababu alikuwa na maumivu makali sana,” akasema mama huyo licha ya Bi Hamisi kumhakikishia kuwa hali yake ilikuwa shwari.

Alisema alikuwa na wasiwasi kwani mwanawe alikuwa amechoka sana.

“Uchungu wa uzazi ulizidi kumchoma. Maji yalipozidi unga mwanangu akaniagiza nimkimbize hospitali ya Gambato. Aliniambia nijitayarishe kumpokea mjukuu wangu siku hiyo,” akaongeza mama huyo.

Alikimbizwa katika kliniki hiyo ya Gombato huku akilia kutokana na maumivu ya ujauzito. Kulingana na Bi Omar walifika katika kliniki hiyo saa 4.30 wakakuta imefungwa. Walimsihi bawabu awafungulie lakini kilio chao kiliambulia patupu.

Mvua ikaanza kunyunyiza, mama huyo akaita majirani waokoe maisha ya mwanawe na mjukuu wake.

“Bawabu alisema hapakuwa na mhudumu wa afya wa kutuhudumia. Akatuelekeza kliniki nyingine. Nilimsihi bawabu amwite mhudumu anayeishi karibu atuhudimie au hata gari la wagonjwa dharura lakini alikataa. Mtoto wangu akapiga magoti akaomba na kukata roho. Sikuamini macho yangu,” ama huyo alisema.

Juhudi za mkunga kumwokoa maisha mama huyo hazikufua dafu kwani alikuwa ashakata roho. Maiti ilikaa nje ya hospitali hiyo ikinyeshewa huku bawabu akikataa kuwaruhusu kuingia kwenye kiliniki hiyo.

 

Alifariki

“Maji yalimwagika, akapoteza ufahamu akaanza kutetemeka na kuaga dunia nikimwangalia na kushindwa namna ya kumsaidia. Nilisimama wima nikiduwaa machozi yakinitiririka, nikiwaangalia wakiniponyoka. Nikamsihi bawabu akubali tuhifadhi maiti kwenye kivuli lakini alikataa,” akasema Bi Omar.

Wakakata tamaa na majirani wakamsaidia kupeleka maiti ya mama huyo na mtoto mchanga nyumbani.

Lakini ilipofika saa moja usiku, mama huyo alisema alishangaa wakati wahudumu wawili wa afya walifika wakiwa wameabiri gari la wagonjwa wa dharura wakitaka kupeleka maiti katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Msambweni.

“Nilichanganyikiwa, nilidhani ilikuwa ndoto mbaya. Yaani mtoto wangu alipokuwa hai gari hilo lilishindwa kuja kumwokoa sasa amefariki gari limefika kumbeba? Maiti ina thamani sana kuliko binadamu hai?” akauliza huku machozi yakimtiririka.

Alihojiwa na wahudumu hao na baadaye wakaondoka.

Bi Omar alisema alilazimishwa kutia saini yake kwenye karatasi malaum ya hospitali hiyo.

“Walitaka kuchukua mwili kuipeleka mochari, nikakataa sababu mimi sijasoma sikuelewa kwanini ninalazimishwa kutia saini. Baada ya kutia saini nilishangaa mhudumu aliposoma maelezo akisema nilikataa mwili ufanyiwe upasuaji,” akaongeza.

Wahudumu hao walichukua kitabu cha marehemu cha kliniki na kuondoka.

Ijumaa wiki hiyo hiyo walizika maiti hizo.

Familia hiyo ilisema kutokana na ufuraka unaokithiri walishindwa kumpeleka Bi Hamisi katika hospitali ya kibinafsi ili kuokoa maisha yake na mtoto wake.

 

Kujiondolea lawama 

Taifa Leo ilipofika hospitali hiyo, wahudumu wa afya walioomba majina yao yabanwe wakihofia kuchukuliwa hatua za kisheria na serikali ya kaunti walisema marehemu alifika hopsitalini wakati walikuwa wameshafunga.

“Kliniki zote za umma nchini zinafungwa mnamo saa 4.30 jioni isipokuwa kama kuna dharura. Mama huyo alifika hapa saa 6pm, tulikuwa tushafunga,” akasema mhudumu huyo.

Mhudumu mkuu Omar Mrenje alisema alikuwa hayuko katika kliniki hiyo wakati mkasa huo ulifanyika.

Lakini Bi Omar alipinga madai hayo akisema walifika hospitalini kabla ifungwe.

Alitoa wito kwa serikali ya kaunti kuchunguza kisa hicho na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua kali.

“Mwanamke mwingine asifariki akijifungua, hii iwe ya mwisho,” akasema Bi Omar.

Daktari mtaalam wa maswala ya uzazi katika hospitali ya Pandya huko Mombasa alisema huenda mama huyo alifariki baada ya kupatikana na tatizo la afya kighalfa.

“Mwanamke mja mzito anaweza kwenda hospitalini lakini baadaye anapoenda kujifungua ghafla anapatikana na matatizo ya kiafya kama kupandwa na shinikizo la damu ama kuvuja damu haya yote yanaweza kuepukika endapo mhusika ataenda hospitalini au kufuata kliniki,” Dkt Marjan akasema.

 

Changamoto

“Wakazi hao ni maskini na mara kwa mara hawaendi kliniki ama wanachelewa kwenda hospitalini. Kando na hiyo pia kuna uhaba wa wahudumu wa afya, ukosefu wa huduma za dharura, hospitali ambazo hazina vifaa, hospitali kuwa mbali, barabara mbovuni baadhi ya changamoto zinazowakabili,” akasema Dkt Marjan.

Majuzi waziri wa afya Bi Sicily Kariuki aliiambia kamati ya seneti ya afya umuhimu wa serikali za kaunti kuwekeza katika huduma za dharura ili kuokoa maisha.

“Serikali inapania kukabiliana na vifo vya mama wajawazito,” akasema Bi Kariuki.

Mkurugenzi wa matibabu Dkt Jackson Kioko, alisema kuna kliniki zengine ambazo zinafungwa mapema sana huku wagonjwa wakiachwa wkaitaabika kutokana na ukosefu wa huduma za afya.

“Wahudumuw a afya wanaenda nyumbani mapema san ahata unashangaa mgonjwa akikuja kliniki nani atamhudumia? Lazima wakazi karibu na kniliki wajue inafungwa saa ngapi na ikifungwa watapokea matibabu wapi,” akawambia magavana mwezi uliopita.

Serikali ya kaunti ya Kwale ilisema inaendeleza uchunguzi wa kisa hicho na wahusika watachukuliwa hatua wka kuchelea kazini.

Bi Hamisi ni miongoni mwa mamia ya wakenya wanaoaga dunia kutokana na utepetepe wa wahudumu wa afya au ukosefu wa dharura za afya.