Makala

KURUNZI YA PWANI: Msikiti wa Riyadha kufundisha dini ya Kiislamu na tamaduni za Pwani

November 21st, 2018 3 min read

Na CHARLES WASONGA

MSIKITI wa Riyadha, na kituo cha mafunzo ya Uislamu, Lamu, Jumanne, (Novemba 20, 2018) ulifungua ukusara mpya katika historia yake kwa kuzindua mpango mkakati ambao utaangazia kazi zake zote tangu ulipoasisiwa mnamo mwaka 1886.

Hii imeleta mwamko mpya katika historia ya kituo hicho ambacho mwaka huu kilitawazwa kuwa turathi ya kitaifa kupitia Makavazi ya Kitaifa.

Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali Afisa Mkuu Mtendaji wa kituo hicho Abubakar Badawy alionyeshesha furaha yake baada ya uzinduzi huo kufanyika katika Makavazi ya Kitaifa, Nairobi na kuongozwa na Waziri wa Michezo na Utamaduni Bw Rashid Echesa.

“Shughuli ya Novemba 20, Nairobi ni mwanzo wa uzinduzi kamili wa mkakati huo ambao utafanyika Lamu kuanzia Desemba 6 wakati wa sherehe za kila mwaka,” akasema

Hafla hiyo muhimu ilihudhuruwa na wasimamizi wa sasa wadhamini, wazee, wasomi na wanachama wengine muhimu wa taasisi hii

Bw Badawy anasema lengo hasa la kituo Riyadha kutoa mafunzo kuhusu elimu ya dini ya Kiislamu na kutoa mafunzo kuhusu tamaduni za Waswahili.

“Kando na mafunzo ya Quran na dini ya Kiislamu, tunafunza matawi yote ya elimu kama vile elimu ya tabia kwa vijana, kuwasaidia watu, na kumfinyanga mwanadamu kuwa kiumbe aliyekamilika,” akasema

“Wale ambao walipata elimu yao katika kituo cha Riyadha ndio walipanda ngazi na kuwa makadhi katika eneo zima la Afrika Mashariki na Kati,” akaongeza

Bw Badawy, ambaye zamani alikuwa Mbunge wa Malindi, anasema kuwa mwasisi wa Riyadha Habib Swaleh Bin Alwi alitoka Comoros kuja Lamu kwa ajili ya kutoa elimu hiyo.

Kituo hicho vile vile kimepata umaarufu mkubwa kwa sababu huandaa sherehe za Maulid ambazo hufanyika katika mwezi wa nne katika kalenda ya Kiislamu.

“Maulid ni sherehe ya kipekee katika Afrika Mashariki kwa sababu hushirikisha watu kutoka pembe zote za ulimwengu wa Kiislamu. Watu hushiriki swala, mihadhara, mashindano ya kukariri vifungu vya Quran na masuala mbalimbli. Zaidi ya watu 10,000 hushiriki kila mwaka,” anaeleza.

Isitoshe, anaongeza Bw Badawy, watu jamii ya Wakikuyu wanaoishi Mpeketoni pia hushiriki sherehe za Maulidi, “kwa sababu duni ya Kiislamu haigui kwa misingi ya dini, kabila, tabaka wala rangi”

Anasema sherehe hizo za Maulid zimepata umaarufu mkubwa kwa sababu huhudhuriwa na watu mashuhuri kutoka pembe mbalimbali ulimwenguni.

Msikiti wa Riyadha, Lamu. Picha/ Wasonga Charles

“Baadhi ya watu hawa, ambao wamewahi kuhudhuria, na kushiriki sherehe hizo, ni aliyekuwa Rais wa Tanzania Ali Hassam Mwinyi, Rais wetu Mheshimiwa Uhuru Kenyatta na Wasomi maarufu kutoka Yemen na Muungano wa Mataifa ya Kiarabu,” Badawy anaeleza.

Itakumbukwa kuwa Rais Kenyatta alihudhuria sherehe hizo mnamo mwaka wa 2016 ambapo aliwapongeza viongozi wa dini ya Kiislamu eneo la Lamu kwa juhudi zao za kuisaidia serikali kufikia malengo yake ya kudumisha amani maeneo hayo.

“Ni fahari yetu kwamba Rais alitambua kwamba wajibu wetu katika Riyadha ni kuhimiza amani na utangamano kama, suala ambalo limekita katika silabasi yetu ya elimu na sherehe za Maulidi,” Bw Badawy akakariri.a.

Anaeleza kuwa ni wakati wa sherehe hizo ambapo kambi kubwa ya matibabu huandaliwa ambapo watu kutoka maeneo mbalimbali hutibiwa maradhi mbalimbali

“Sherehe za mwaka huu zitafanyika kwa siku tatu, kuanzia Desemba 6 hadi 9 sambamba na kambi ya matibabu. Zaidi ya madaktari 40 wenye ujuzi katika nyanja mbalimbali za utabibu watawahudumia watu katika kipindi hicho cha siku tatu,” Bw Badawy anasema.

“Kutakuwa na watalaamu wa upasuaji, madaktari wa meno, na wengine ambao watatoa huduma zao bila malipo kando na kupeana dawa,” anafafanua.

Falsafa inayoongoza kambi ya matibabu na imenawiri inatokana na hali kwamba mwinzilishi wa Riyadha, Habibu Swaleh Bin Alwi alikuwa na ni tabibu mtajika wakati wa uhai wake.

Katika kitengo cha mafunzo ya tamaduni za Waswahili, kituo cha Riyadha hufundisha, ushairi, ngoma za kitamaduni pamoja na fani mbalimbali ambazo asili yazo ni kisiwa cha Lamu

“Hii ni mojawapo ya sababu zinazoifanya kituo cha Riyadha kuwa kivutio cha watalii katika ukanda wa pwani. Wageni huja kujionea utajiri wa tamaduni za Swahili pamoja na kujifunzo mengi kuhusu historian a chimbuko la kituo hicho maarufu,” Badawy anasema

Naye mwenyekiti wa Riyadha Ahmed Badawy Swaleh Jamalleli anasema makusudio yake mapya ni kuwa kiungo muhimu katika kufanikisha maendeleo na urathi katika eneo hili na hutupa nguvu mpya za kumiliki na kuwajibikia taasisi hii kwa kuhuisha madhumuni yake.

“Ili kufanikisha haya, ni sharti tubuni miradi itakayohusisha jamii yenye wakazi wa aina tofautitofauti mbali na Lamu katika juhudi za kuhakikisha kwamba Riyadha imepata maendeleo endelevu,” anasema katika taarifa.

Hatua hii, anaongeza, ni pamoja na ushirikiano wa Riyadha na taasisi nyinginezo, wafadhili na wahisani wengineo.