KURUNZI YA PWANI: Ujenzi wa mnara wa Wameru wapingwa

KURUNZI YA PWANI: Ujenzi wa mnara wa Wameru wapingwa

Na KALUME KAZUNGU

AZIMIO la jamii ya Wameru kutaka kujenga mnara maalum wa kumbukumbu ya chimbuko lao katika Kaunti ya Lamu limekumbwa na vikwazo kutoka kwa baraza la wazee wa jamii asili za Lamu.

Baraza hilo limetaja jamii ya Wameru kuthibitisha kwanza kwamba ni kweli jamii hiyo iko na mizizi yake eneo hilo.

Wazee hao wanataka jamii ya Wameru kutaja angalau mzee wao mmoja aliyemulikwa katika vitabu vya kihistoria kuhusiana na kuishi kwake Lamu kama inavyodaiwa kwa sasa.

Januari 2020 Kaunti za Meru na Tharaka Nithi zilitangaza mpango wa kununua kipande cha ardhi katika Kisiwa cha Manda ili kujenga mnara huo ambao pia watautumia kama eneo la ibada wakati wakikumbuka historia yao Lamu.

Jamii hiyo inaamini kuwa wakati mmoja katika historia ilijipata imetekwa nyara na kuzuiliwa katika sehemu kwa jina Mbwaa, ambayo inaaminika katika ulimwengu wa leo kuwa Lamu.

Lakini sasa, wazee wa Lamu wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti wao, Bw Mohamed Mbwana wamepinga vikali uhusiano wowote wa Ameru na historia ya Lamu.

Bw Mbwana anasema hawajaona hata kitabu kimoja kilichotaja jamii ya Wameru kuwa na chimbuko lao Lamu.

Kwa msingi huu, alisema hawako tayari kuruhusu jamii hiyo ya Ameru kujenga mnara wa chimbuko lao la kihistoria hadi pale watakapofaulu kudhihirisha kweli jamii hiyo ina uhusiano wowote na eneo hilo.

“Tumeshangaa kusikia kwamba magavana wa Meru na Tharaka-Nithi wanatafuta ardhi Lamu kujenga mnara wa chimbuko la historia yao Lamu. Kwa nini wafanye hivyo na hakuna hata kitabu kimoja kilkichoorodhesha jamii ya Wameru kuwa na chimbuko lao hapa Lamu,” akasema.

Kulingana naye, vitabu vya kihistoria walivyotumia kufanya utafiti vilitaja tu Waswahili, Waarabu na Wareno ambao kwa wakati mmoja katika historia walijipata mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki, kuwa na chimbuko lao Lamu.

“Ikiwa Wameru hawatataja hata mzee mmoja wao aliyeorodheshwa katika historia ya Lamu, basi hatutawakubalia kujenga mnara wao hapa,” akasema Bw Mbwana.

Licha ya hayo, Mwenyekiti wa Jamii ya Wameru, Kaunti ya Lamu, Bw Jacob Muroki, alishikilia kuwa pendekezo la Wameru litaafikiwa kwani ni kweli jamii hiyo iko na uhusiano wa dhati na eneo hilo. Bw Muroki aliwashauri wanachama wa Baraza la Wazee wa Lamu kukoma kuingiza siasa katika mambo ambayo yako wazi.

“Kwa nini Baraza la Wazee wa Lamu linakimbilia kuupinga mpango huo? Ameru wako na chimbuko lao Lamu na hakuna wa kupinga hapo. Ninachoshuku ni kwamba hao wazee kuna uwezekano hawajasoma ipasavyo. Warudi tena kwenye vitabu. Mnara lazima ujengwe Lamu,” akasema Bw Muroki.

Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee, Bw Mohamed Athman alilitaka Shirika la Kitaifa la Makavazi na Turathi (NMK) kutafuta ushauri na maafikiano kati ya serikali za Kaunti za Lamu, Meru na Tharaka-Nithi kabla ya hatua yoyote kuchukuliwa kuhusu ujenzi wa mnara huo.

Kwa upande wake, Mzee Said Seif alisema huenda mpango wa kujenga mnara wa chimbuko la historia ya Wameru eneo la Lamu una lengo la kisiasa.

“Wanataka kulazimisha kuhusishwa na historia ya Lamu ili wapate sauti ya kisiasa eneo hili. Isitoshe, ninahisi mpango huu unanuiwa kusaidia ardhi za Lamu zinyakuliwe na hatutakubali. Tayari tumechoshwa na dhuluma za kihistoria ambazo zimekuwako Lamu tangu jadi,” akasema Bw Seif.

You can share this post!

Akatwa kidole na aliyenyemelea mkewe

UDAKU: Difenda Tomori Fikayo na msupa Geordie Amber Gill...

adminleo