Makala

KURUNZI YA PWANI: Wakazi wahimizwa wajiandae hali ya kawaida ikitarajiwa

May 26th, 2020 2 min read

Na MISHI GONGO

ENEO la Pwani limeanza mikakati ya kujitayarisha kurejea kwa hali ya kawaida kama alivyodokeza Rais Uhuru Kenyatta wiki iliyopita.

Akizungumza na wanahabari Jumatatu, mshirikishi wa usalama katika eneo la Pwani Bw John Elungata alisema ni wakati mwafaka wa sekta mbalimbali kuanza matayarisho ya kurejea kwa hali ya kawaida siku chache zijazo.

Bw Elungata aliwahimiza wamiliki wa hoteli kuanza kuandaa matayarisho ya kuwakaribisha watalii.

“Wamiliki wa hoteli wamekuwa na muda wa kutosha kurekebisha hoteli zao ili kuanza kupokea wageni pale nchi itakapofunguliwa,” akasema Bw Elungata.

Wiki iliyopita Rais Kenyatta alitangaza kuwa serikali italegeza marufuku ili kufufua uchumi ambao umedorora kutokana na athari hasi za Covid-19.

Rais Kenyatta alieleza kuwa nchi haiwezi kuendelea kujifungia.

Alisema ugonjwa utakuwa nasi kwa muda kabla ya kudhibitiwa vilivyo.

Bw Elungata alisema miongoni mwa matayarisho wanayoweka ni kuchimba visima 15 katika kaunti za Kilifi, Kwale na Mombasa ambazo zina idadi kubwa ya maambukizi ili kuhakikisha kuwa wakazi wanapata maji ya kutosha.

Aidha Bw Elungata alisema vijana 18,000 wataandikwa kuhakikisha kuwa wanachunga wanyamapori.

“Vijana wasipoajiriwa katika shughuli hii, wanyamapori ambao ni kivutio kikuu cha utalii watakuwa katika hatari,” akasema.

Alisema shule zitapanuliwa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakuwa katika mazingira mazuri watakaporudi shuleni.

Bw Elungata pia alisema serikali inapanga kujenga daraja katika kivuko cha feri, ambalo litasaidia kupunguza msongamano unaoshuhudiwa kwa sasa.

“Daraja litakuwa na uwezo wa kufunga na kufunguka ili kuwezesha meli kupita, lakini ujenzi wake utachukua muda wa miezi sita ndipo likamilike. Daraja hili litasaidia kudhibiti virusi vya corona kwani litaruhusu wakazi kuekeana nafasi,” akasema.

Hata hivyo Bw Elungata aliwatahadharisha wakazi kuwa zuio na kafyu vikishaondolewa, ni muhimu waendelee kuzingatia masharti yaliyowekwa ili kudhibiti kueneo kwa ugonjwa huo hatari.

“Mikahawa na sehemu za burudani zitafunguliwa lakini tutapaswa kuendelea kuzingatia masharti yaliyowekwa kama kuvaa barakoa ili kujikinga,” akasema.

Aidha alisema magari ya usafiri wa umma yatalazimika kutobeba abiria kupita kiasi.

“Maisha yatageuka; hayatakuwa kama awali. Tutalazimika kuendelea kuvaa barakoa na kuekeana umbali baina ya mtu na mwenzake,” akasema mshirikishi huyo.

Pia alisema barabara zilizoharibika kufuatia mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa katika kaunti za Taita Taveta na Tana River zitakarabatiwa.

Aliongezea kuwa vijana wanaosafisha mitaa watapata Sh3,000 kwa siku kutoka kwa serikali.

“Pesa hivi tunatumai kuwa zitawasaidia katika kujiendeleza kiuchumi na pia kusafisha mazingira. Haya yote ni kuhakikisha kuwa uchumi wetu unarudi pale ulipokuwa kabla kuzuka kwa ugonjwa huu,” akasema.