Makala

KURUNZI YA PWANI: Wanawake wa jamii ya ufugaji wakumbatia elimu ya ngumbaru

September 10th, 2018 4 min read

Na STEPHEN ODUOR

MASOMO ya mtoto wa kike katika familia za wafugaji katika Kaunti ya Tana River hayajatiliwa maanani, na kuchangia kwa wengi kuozwa wakiwa na umri mdogo.

Kulingana na tamaduni zao, baada ya mtoto wa kike kukeketwa, huwa keshakuwa mwanamke na hivyo tayari kuolewa.

Kulingana na idara ya watoto katika kaunti, takriban asilimia 85 ya wanawake walio katika ndoa katika jamii za wafugaji huolewa wakiwa na kati ya miaka 12 na 24.

Hivyo basi baadhi ya wanawake katika jamii hizi huwa hawana ujuzi wa kusoma wala wa kuandika.

Lakini mambo sasa yameanza kubadilika kwani baadhi ya wanawake wameamua kujiunga na elimu ya watu wazima almaarufu ngumbaru.

Fatuma Gafo, mkaazi wa bura ni mama wa watoto sita na aliyekuwa mke wa pili wa mumewe aliyemtaliki alipogundua amejiunga kisiri na masomo ya gumbaru mwaka uliopita.

“Nilianza kuungana na mama fulani mjane aliyekuwa anaenda kusoma masomo ya watu wazima kule mtaani, nikaanza kwenda kusoma na hapo mume wangu alipogundua, akaamua kunitaliki, ” asimulia.

Mume wake alimshtaki kwa wazee kwa kuungana na wanawake wa ‘kutangatanga’ na wanawake wasio na tabia njema, wala heshima kwa ndoa, na hata kumsingizia kuwa kahaba.

Hata hivyo, Bi Gafo aliikubali talaka hiyo, kwani hata hivyo alikuwa ametelekezwa kama mke wa pili, na kila kitu kupewa mke wa nne, hivyo basi hapakuwa na sababu ya kusalia katika ndoa ile.

“Mimi nilisahaulika kitambo sana, hata watoto niliachiwa na mapenzi alipatia mke mdogo, nilisalia gogo tu na yeye kunitaliki ilikuwa mbinu nyingine tu ya kutengeza nafasi ya mke mwengine, ” alieleza.

Alirudi kwao na watoto wake sita, na kila waliporauka kwenda skuli, aliandamana nao moja kwa moja, wote wakiingia darasani, ila kwake, aliingia darasa la watu wazima.

Amekuwa akijizatiti darasani, kwani aliingia akiwa hajui kusoma, kuandika, wala kuzungumza Kiswahili vizuri, lakini sasa anaweza hata kuandika majina ya wanawe.

“Mimi sikujua hata kuandika jina langu, hata Kiswahili kilikuwa shida sana, ni Kiorma tu nilichoelewa, lakini sasa mambo ni tofauti kwangu, saa hizi naandika hata sentensi nzima,” anaeleza kwa tabasamu.

Bi Gafo sasa ana furaha tele, kwani anahisi amepata uhuru ambao alinyimwa tangu utotoni.

Baba yake aliaga miaka mitano iliyopita, na sasa amebaki na mama yake ambaye anamsaidia na malezi, na hata kumpa motisha katika juhudi zake.

Akiwa na umri wa miaka 26 sasa, Bi Gafo atakuwa anajiunga na darasa la kwanza, akiwa na imani ya kusukuma gurudumu hilo la masomo hadi chuo kikuu, majaliwa.

“Nimeanza na nia yangu ni kufika chuo kikuu, nami niwe kielelezo na mfano wa kutajika katika jamii,” alieleza.

Hamisa Dhofar Bile ni mwingine anayejizatiti katika kuhakikisha kuwa gurudumu la masomo linaelekea kileleni.

Aliolewa akiwa na miaka 13 pindi tu alipomaliza darasa la nane kwa mzee wa miaka 56, aliyekuwa na wake wawili baada ya kutaliki wengine wawili.

“Ni mzee niliyemjua nikiwa mtoto na hata nikiwa nabaleghe, kila alipooa tulihudhuria sherehe za harusi na kula kweli kweli,” anasimulia huku akicheka.

Bi Bile alishuhudia harusi mbili za mwanamume huyo na hata baadhi ya watoto wa mzee huyo walisoma pamoja katika shule ya msingi.

Vivyo hivyo alishuhudia mwanamme huyo akiwataliki wake wake wawili.

Kuolewa kwake hapakuwa na fursa ya kuchagua, kuwaza wala kuamua, bali kutii amri ya babake ambaye anaeleza kuwa hangechelewa kuua yeyote aliyepinga uamuzi wake.

“Babangu hakuwa mtu wa kuwaza na mwanamke, hata ubishi wa majirani ungemtia wazimu kiasi cha kuingilia kati kumcharaza mwanamke; aliogopewa sana, alipotoa amri, wewe ni kutii, ” asimulia.

Mbali na kuwa alikuwa amesoma kiasi na kujua kuandika na kusoma, Bi Bile alikuwa mwana mitindo na alipenda sana kutunga nyimbo na kuimba.

Ndoa ilikuwa starehe tele mwanzoni, mapenzi yalikolea utamu hadi pale, alipojipata katika nafasi ya mke wa kwanza baada ya wenzake kupewa talaka zao kwa sababu tofauti tofauti.

“Nilishtukia niko hapo juu, wenzangu walikuwa wameachwa na wakawa wanaishi kivyao makwao, na hapo nikajua hata nami zamu yangu haikuwa mbali sana, ” alisimulia.

Haikuchukua muda, mume wake alijipa jiko jingine la miaka kumi na sita, msichana aliyekinai masomo akiwa kidato cha pili.

Bi Bile wakati huo alikuwa na watoto wawili na akawa amedungwa kisiri sindano ya kupanga uzazi kwa ushauri wa wenzake waliokuwa wametalikiwa.

Sababu ya mume wake kumwacha ilikuwa ni kuwa hakuwa anazaa tena, na hivyo akamwona ovyo.

Baada ya muda mchache mune wake alimfanya goma, kumpiga kila jioni na haswa alipojiunga na wenzake katika hafla za kitaifa katika jukwaa la Hola, ambapo walikuwa wakiimba kama kikundi.

“Alisema kuwa nilikuwa naenda kufanya ukahaba, kujionyesha mbele ya watu wenye pesa ili wanifuate, wanitongoze na akawa ameeka wanaume kunichunguza, salamu kwa mwanammw yeyote ilichangia kipigo zaidi, ” alisimulia.

Kipigo kilipozidi Bi Bile aliomba talaka yake, jambo ambalo kidogo tu lingesababisha kifo chake usiku ule isingekuwa imani ya mke mdogo aliyemtuliza mume yule kwa maneno matamu.

Aliingilia kati na kumtuliza mume yule na kumtoa pale, akaenda kumzuzua kwa mapenzi na kumtia kiburi katika harakati za kumshawishi kutoa talaka bila kusababisha fujo zaidi.

Asubuhi ile, mwanamme yule aliamka na kwa hasira akampa talaka.

“Alinipa talaka tatu, na mimi nikashukuru Mungu, nikachukua watoto wangu wawili, mzigo mwepesi hata sikurudi kwetu, nilianda kwa kakangu Garissa,” alieleza.

Akiwa Garissa alipata fununu kuhusu shule ya gumbaru na baada ya kushawishiana na kakake ambaye alikuwa mfanya biashara pale, alimruhusu kujiunga na chuo.

“Kakangu alinipenda sana, angefanya lolote kuniona niko na furaha, hata shule alinisindikiza, ni mtu tofauti na babangu kama shilingi na pesa ya noti,” anaeleza.

Amekuwa akisoma katika shule ya gumbaru kwa muda wa miaka miwili sasa, akiwa katika kiwango cha shule ya upili, kidato cha pili.

Pia amekuwa mmoja wa wanaharakati wa kupinga dhuluma dhidi ya mtoto wa kike, haswa maswala ya elimu na ndoa za mapema.

“Nina watoto wa kiume, wamekuwa sasa, na kila siku nawafunza kuwa watiifu, na kuheshimu wenzao wa kike, hata kakangu anayewasomesha anawafunza kuwa wanaume kamili,” anaeleza.

Bi Bile amependa sana somo la bayolojia, historia na kiingereza,na hata anawazia kuwafunza wanawake wenzake madhara ya ukeketaji kupitia ufahamu wa masomo ya sayansi na historia.

Akiwa na umri wa miaka 27,naazimia kujinga na chuo kikuu na kusomea udakitari, na kuwa kielelezo kwa jamii.

Wanawake hawa wawili ni wachache kati ya hamsini na tatu ambao wamejiunga na shule za gumbaru katika kaunti ya Tana River.

Baadhi yao wakiwa wametalikiwa na wengine wakiwa wameachwa wajane katika umri mdogo.

Wako katika viwango tofauti tofauti katika kisomo, lakini nia yao ni kulibingirisha gurudumu la masomo hadi ngazi zake za juu, na kuandikisha historia mpya ya maisha yao na hata kwa kizazi chao.

Mbali na kuwa kuna pingamizi kutoka kwa wanaume, wanawake hawa wanajizatiti kuhakikisha kuwa juhudi zao, zinaleta kudura.