HabariSiasa

Kushtakiwa kwake Rotich kulimuanika Ruto na wafuasi wake

July 28th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Kushtakiwa kwa aliyekuwa waziri wa fedha Henry Rotich, maafisa wa wizara hiyo na wale wa mamlaka ya maendeleo ya bonde la Kerio (KVDA), kuhusiana na sakata ya mabwawa ya Arror na Kimwerer, kumemuabisha Naibu Rais William Ruto ambaye aliwatetea vikali akidai hakuna pesa zilizopotea.

Uchunguzi ulipokuwa ukiendelea, Dkt Ruto aliutaja kama feki na kumlaumu Mkurugenzi wa upelelezi wa jinai (DCI) George Kinoti na mwenzake wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji kwa kutumiwa kisiasa kulemaza ujenzi wa mabwawa hayo.

Zaidi ya mara mbili, akiwa mbele ya Rais Kenyatta na hata Jaji Mkuu David Maraga, Bw Kinoti na Bw Haji, Dkt Ruto alidai pesa zilizokuwa zimelipwa mwanakandarasi aliyeshinda zabuni ya kujenga mabwawa hayo katika kaunti ya Elgeyo Marakwet zilikuwa Sh7 bilioni tu na sio Sh21 bilioni alivyodai Bw Kinoti.

Alisisitiza kuwa pesa hizo hazingepotea kwa sababu zilikuwa zimewekewa dhamana ya benki.

Dkt Ruto aliapa kwamba mabwawa hayo yangejengwa na kukamilika licha ya kubainika kuwa kampuni ya CMC di Ravenna iliyopatiwa kandarasi hiyo ilikuwa imefilisika.

Licha ya miito ya kumtaka asubiri uchunguzi ukamilike, Dkt Ruto aliendelea kumkashifu Bw Kinoti na wakati mmoja wandani wake walimtaka mkurugenzi huyo aachie Tume ya Maadili na kupambana na ufisadi (EACC) uchunguzi wa madai ya uhalifu wa kiuchumi.

Wadadisi wanasema kwamba kushtakiwa kwa Bw Rotich na maafisa wa KVDA kuhusiana na sakata hiyo ni sawa na kumpiga kofi Dkt Ruto usoni machoni mwa umma.

“Ruto hana pa kujificha kwa kutetea ufisadi. Ukiangalia matukio ya hivi majuzi na hasa kuhusu sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwerer utagundua kwamba alikuwa akifahamu kilichotendeka na ndio sababu alikuwa akiwatetea washukiwa,” alisema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Anataja matamshi ya Dkt Ruto alipohutubia kongamano la ugatuzi kaunti ya Kirinyaga kwamba alikuwa mhusika katika mabwawa hayo kama yaliyomuanika zaidi.

“Dkt Ruto alikosea kwa kupiga vita idara ya upelelezi ilipokuwa ikichunguza sakata hiyo. Alijaribu kuwalinda washukiwa lakini hakufaulu na hii imemuacha pabaya,” asema.

Kwenye kongamano hilo, Dkt Ruto alipuuza waliomlaumu kwa kutetea mradi huo akisema ni sawa na kuuliza fisi sababu ya kutaka kuvamia kundi la mifugo.

Wandani wake, akiwemo seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, mwenzake wa Kericho Aaron Cheruiyot na wabunge Oscar Sudi na David Rono wamekuwa wakimtetea na kumlaumu Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kumpiga vita naibu rais ili kuzima azima yake ya kuwa rais 2022.

Bw Kamwanah anasema Dkt Ruto anafaa kujiandaa kwa mashambulio makali zaidi kutoka kwa wapinzani wake wa kisiasa.

“Watatumia sakata hiyo kuendelea kumsawiri kama kiongozi anayewatetea wafisadi. Atakuwa na wakati mgumu sana. Makosa aliyofanya ni kukashifu idara huru za uchunguzi, kukaidi mkubwa wake (Rais Kenyatta) ambaye ametangaza vita dhidi ya ufisadi,” alieleza.

Kulingana na mwenyekiti wa chama cha ODM, John Mbadi, Dkt Ruto na Bw Murkomen ambaye ni kiongozi wa wengi katika seneti anafaa kujiuzulu kufuatia kushtakiwa kwa Bw Rotich na maafisa wa KVDA kuhusiana na sakata ya ujenzi wa mabwawa hayo.

“Naibu Rais Ruto na vibaraka wake akiwemo Murkomen walijitokeza hadharani kusema hakuna pesa zilizopotea. Hatua ya DPP ya kuwafungulia mashtaka washukiwa imemuanika Dkt Ruto na seneta huyo. Wanafaa kuomba msamaha kwa kuwapotosha Wakenya,” Bw Mbadi alisema.

Wadadisi wanasema kushtakiwa kwa washukiwa hao kutazidisha malumbano kati ya mirengo ya Kieleweke na Tangatanga ya chama cha Jubilee. Tangatanga inamuunga Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta 2022 na Kieleweke unampinga vikali.

Mmoja wa wanachama wa Kieleweke mbunge wa Cheragany, Joshua Kutuny alisema kushtakiwa kwa washukiwa kuhusiana na sakata hiyo ni pigo kwa wanaotetea ufisadi.

“Hatua ya DPP inafaa kukumbusha wale wanaotetea ufisadi kwamba wataanikwa. Uchunguzi ulipokuwa ukiendelea, walimkashifu DPP na DCI lakini ushahidi umewaanika. Hawafai kupotosha watu kwa kudai jamii fulani inalengwa. Hivi ni vita dhidi ya ufisadi,” alisema Bw Kutuny.

Mwanachama mwingine wa mrengo wa Kieleweke Ngunjiri Wambugu alisema uchunguzi ulibainisha kuwa Bw Kinoti hakuwa akitumiwa kisiasa Dkt Ruto alivyodai kwa sababu ilibainika pesa zilipotea.

Mbunge huyo wa Nyeri mjini alisema madai ya Dkt Ruto na wandani wake yalilenga kutisha wapelelezi wakomeshe uchunguzi ambao uliwapeleka ng’ambo kufuatilia jinsi pesa zilivyolipwa, zabuni ilivyotolewa na waliohusika.

Wadadisi wanasema kwamba kauli za wandani wa Dkt Ruto baada ya kushtakiwa kwa washukiwa wa sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer zinaweza kumwanika zaidi.

Mnamo Jumatano, mbunge wa Kapsaret, Oscar Sudi alimshambulia Rais Kenyatta kufuatia kukamatwa na kushtakiwa kwa Bw Rotich na kumtaka ajiuzulu.

Kulingana na Bw Ben Makali, mdadasi wa siasa, Dkt Ruto na wandani wake wanajiharibia kwa kuendelea kupinga vita dhidi ya ufisadi.

“Dkt Ruto anafaa kuwazima wandani wake waache kupinga vita dhidi ya ufisadi. Hii inamfanya aendelee kutengwa serikalini. Anafaa kunyenyekea kwa mkubwa wake Rais Kenyatta na kukumbatia handisheki. Hauwezi ukashindana na serikali unayohudumia,” aeleza.

Bw Sudi mwenyewe alikiri kuwa hali ni mbaya kwa Dkt Ruto. “Hii inaudhi sana. Niliuliza Rais kama kuna mahali wamekosana na William wasuluhishe mambo yao lakini mambo yanaelekea kuwa mabaya,” Bw Sudi alisema alipohutubia wanahabari nyumbani wake Jumatano.