Makala

'Kusuka mabinti na kuwarembesha kucha ni riziki tosha'

June 25th, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

Ususi ni mojawapo ya gange inayoaminika kupaswa kufanywa na wanawake pekee, kwa kuwa ni kazi inayohusisha wateja wa jinsia ya kike.

Hata hivyo, dhana hiyo sasa imeonekana kupitwa na nyakati, vijana jinsia ya kiume wakiichangamkia na kuigeuza kuwa mtandao wa kuzimbua riziki.

Molo Market, soko lililoko katika kaunti ya Nakuru, saluni Jimmy Wa Cutex ina sifa za kipekee kutokana na umaarufu wake katika shughuli za kusuka na kurembesha wanawake.

James Wa Wanjiru ndiye mwasisi na mmiliki wa ‘karakana’ hiyo ya kurembesha kina dada, aliyoianzisha mwaka uliopita, 2019. Ikizingatiwa kuwa ni msusi wa jinsia ya kiume, wateja hufurika kupata huduma zake.

“Eneo hili wengi hawajaona wanaume wakisuka, ni jambo linalowavutia, hatua inayochangia kuimarisha huduma ninazotoa,” James anasema.

Ikiwa ni ndoto yake kuwekeza katika sekta ya biashara, kijana huyu anasema kufungua saluni hiyo ilikuwa mojawapo ya maazimio yake maishani. Ndoto hiyo haijaanza leo wala jana, ila miaka kadhaa iliyopita.

Kwa sababu ya ukosefu wa karo, James, 28, anasema alisoma hadi darasa la nane, ambapo alifanya mtihani wa kitaifa KCPE mwaka wa 2008. “Wazazi hawakuwa na uwezo kifedha, na nililazimika kutafuta vibarua vya hapa na pale kukithi riziki na kujiendeleza kimaisha,” anaelezea, akifichua kwamba alikita kambi Kericho ambapo aliajiriwa kuuza soseji na matunda.

James anaendelea kueleza kwamba iwapo kuna jambo lililomtia motisha, ni kuona mwajiri wake akipokea mapato ya mauzo aliyofanya mchana kutwa. “Japo mshahara ulikuwa duni, nilitamani sana wakati mmoja kumiliki biashara,” anasema.

Kijana huyu anasema alikuwa na mapenzi ya dhati katika safu ya sanaa, kupaka kucha za wanawake hina, rangi na kuzinakshisha. Kulingana na James, uchoraji ni kipaji alichojaaliwa na Mungu, ambapo akiwa shuleni anasema aliishia kuvurugana na walimu kwa kile anataja kama “kurembesha vitabu kwa kuchora vibonzo kwa wino”.

Ni kazi ya mikono, macho na kutumia bongo kuimarisha ubunifu na hatimaye aliiingilia. Katika harakati hizo, ususi ulianza kumvutia.

Mnamo 2017, kwa mtaji wa Sh50 pekee anazosema alitumia kununua kichana, alianza ususi tamba. “Kunakshisha kucha inaenda sambamba na ususi, hivyo basi nilijumuisha huduma hizo,” anadokeza.

Ni safari iliyokuwa na milima na mabonde, akisema changamoto kuu ilikuwa kutoza mteja nauli ili kumfikia. Aidha, alivumisha huduma zake kupitia mitandao ya kijamii, Facebook – Jimmy Wa Cutex ikiwa nembo maarufu kwa watumizi. “Baada ya kusuka wateja, nilipiga picha za staili na mitindo niliyofanya na kuzipakia mitandaoni zikiandamana na nambari za rununu,” anasema.

Jitihada hizo ndizo zilifanikisha James kufungua saluni yake eneo la Molo 2019, kwa mtaji wa Sh30, 000 alizoweka kama akiba kupitia huduma tamba. Kufikia mwezi Desemba, msusi huyu anasema kiwango cha mapato kilikuwa kimefika faida isiyopungua Sh2, 000 kwa siku.

Ni mjasirimali aliyebuni nafasi za ajira kwa vijana, na kufikia sasa ana wafanyakazi wanne. Licha ya kuwa alitamani kuwa mwandishi na mtangazaji wa habari ila karo ikakosekana kujiendeleza kimasomo, anajivunia kuwa katika sanaa ya ususi na urembeshaji wa wanawake, akifichua kwamba ameweza kuhudumia watangazaji tajika nchini.

“Ninashauri vijana wapalilie talanta walizojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Ajira za afisi ni haba, kupitia vipaji vyetu tunaweza kubuni kazi,” James anahimiza, akisema kuna vipaji wengi mno nchini na serikali inapaswa kuwapiga jeki na kuwahamasisha.

“Serikali ifanye hamasisho vijana watumie talanta walizojaaliwa kujiimarisha kimapato na kimaisha. Kikwazo kilichopo ni ukosefu wa fedha kati yao, hivyo basi iwapige jeki,” anaeleza msusi huyo.

Staili na miundo ya ususi anayofanya ni pamoja na braids, weave, retouch dreads, lines, kulainisha nywele, kuzipaka rangi, miongoni mwa zingine. Huduma zingine ni kama vile; Pedicure, manicure, cutex na gel polish.

Ususi na huduma zake, zinagharimu kati ya Sh100 – 2, 000.

Wakati wa mahojiano, James alisema janga la Covid – 19 limeathiri kwa kiasi kikuu biashara yake. Alisema kiwango cha wateja kimeshuka kwa asilimia 70.

“Watu (akimaanisha wateja) wanaogopa kusukwa kwa sababu hawajui nilisuka nani awali, kwa hofu ya kuambukizwa virusi vya corona,” akasema, akiongeza kueleza kwamba amezingatia taratibu, vigezo na masharti ya wizara ya afya kuzuia maambukizi ya virusi hivi hatari.

Kilio chake kinawiana na cha Samuel Karanja, msusi tajika kaunti ya Nairobi, ambaye anasema amelazimika kufunga saluni yake. “Ninaifungua kupitia oda. Corona imeathiri utendakazi kwa kiasi kikuu,” analalamika.