Makala

Kutana na Mboni wa kwanza ambaye ni polisi kupata Shahada ya Digrii

August 22nd, 2024 2 min read

SAFARI ya kutia moyo ya Bw Mohamed Nyatta, ilianza alipozaliwa na kukua katika kijiji cha mbali cha Bar’goni, Lamu Magharibi.

Kijiji hiki ni mojawapo ya vijiji vilivyo katika msitu wa Boni, ambapo hali ya maisha huwa ngumu kiasi cha kwamba elimu huathirika kila muhula.

Hii ni kutokana na hali kuwa walimu huchelewa kurudi shuleni muhula unapoanza kwani lazima wasubiri kupelekwa kwa ndege ya kijeshi, nao wanafunzi wa shule za upili pia husubiri ndege kuwasafirisha kutoka vijijini.

Hali ya usafiri wa barabarani ni mbovu na hatari kwa sababu ya mashambulio ya kigaidi.

Bw Nyatta anamshukuru Mungu akitaja nidhamu, bidii na uvumilivu kama nguzo kuu za mafanikio yake ya kupambana hadi akawa mwenyeji wa kwanza anayejulikana katika kijiji hicho kupata shahada ya digrii.

Bw Nyatta alisoma katika Shule ya Msingi ya Mokowe Arid Zone iliyoko Lamu Magharibi 1997, umbali wa takriban kilomita 30 kutoka nyumbani kwao kijijini.

Baadaye alijiunga na Shule ya Upili ya Ganze katika Kaunti ya Kilifi hadi 2009.

Katika azma ya kuongeza masomo zaidi, alijiunga na Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM) ambako alisoma na kufuzu kwa Shahada ya Kwanza katika uanahabari.

Bw Nyatta, 33, anamkumbuka marehemu mamake Mariam Babito Kololo, pia mzaliwa wa msitu wa Boni kwa kujitolea kuhakikisha watoto wake wanapata elimu.

“Kwa kusema ukweli, yeye ndiye sababu ya maisha ya kisasa ninayoishi leo. Alinitayarisha kwa ajili ya kazi kubwa iliyo mbele yangu katika maisha haya kwani alipanda maadili na fadhila ambazo hadi sasa zinaishi ndani yangu. Apumzike kwa amani,” akasema Bw Nyatta.

Pia anatambua juhudi za wasimamizi wa eneo la ndani ya Lamu, akiwemo Kassim Athman Hassan, almaarufu Chifu Apollo ambaye alimuunga mkono kamili katika safari yake ya elimu na kumweka katika ulimwengu wa kweli.

Akigusia sekta ya elimu miongoni mwa jamii ya Waboni, Bw Nyatta anasema mengi yanafaa kuwekwa.

“Ndoto ni kubwa zaidi kwa mtoto wa Boni katika suala la elimu. Ninaamini kizazi cha sasa cha Aweer/Boni kinakumbatia elimu kweli. Hii inapaswa kuleta mabadiliko katika siku zijazo. Kuna mwanga mwishoni mwa handaki,” akasema Bw Nyatta.

Mnamo 2016, mwaka mmoja tu baada ya kuhitimu, Bw Nyatta alipokea mafunzo ya polisi katika chuo cha Kiganjo kwa miezi tisa.

Leo, Bw Nyatta ni afisa wa polisi katika Kituo cha Polisi cha Diani, Kaunti ya Kwale.

Anasisitiza kuwa bado ana mengi ambayo anatakiwa kuyafanikisha kwa sasa baada ya kusajiliwa katika Huduma ya Polisi.

Msimamizi wa Wadi ya Msitu wa Basuba-Boni, Azani Ali Rufi alithibitisha kwamba kwa hakika, Bw Nyatta ndiye anafahamika kama mwenyeji wa kwanza wa jamii ya Waboni kupata shahada.

Kulingana na Bw Rufi, mzaliwa mwingine aliyefikia viwango hivyo vya elimu ni Bi Asha Abdalla Kombo ambaye alisomea Shahada ya Biashara na kufuzu muda mfupi baada ya Bw Nyatta.

Bi Abdalla, 34, aliambia Taifa Dijitali kwamba yeye ndiye aliyemsajili Bw Nyatta katika chuo cha TUM mnamo Septemba 2012 alipokuwa akijiunga kusomea Shahada yake ya Kwanza.

Akiwa na Stashahada (Diploma) wakati huo, Bi Abdalla alikuwa akihudumu kama karani katika chuo hicho.

Alipomwona Bw Nyatta akiendeleza masomo yake, Bi Abdalla alitiwa moyo kufanya vivyo hivyo.

“Nilipomsajili alipokuja kusomea Shahada ya Uanahabari, nilipata msukumo wa kusomea shahada. Nilihitimu mwaka wa 2017 ikiwa ni miaka miwili baada ya Nyatta kumaliza masomo katika taasisi hiyo hiyo,” alisema Bi Abdalla.

Bw Rufi alitoa wito kwa jamii ya Waboni kutupilia mbali maisha yao ya kitamaduni na badala yake, watafute elimu na kukumbatia usasa kwa manufaa yao wenyewe.

Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Lamu, Bw Zachary Mutuiri, pia alithibitisha kwamba Bw Nyatta ni miongoni mwa Waboni wachache sana kupata elimu ya juu ambao wengi huwa na Diploma.

“Juhudi zinaendelea ili elimu ya Msitu wa Boni iimarishwe katika miaka ijayo,” akasema Bw Mutuiri.