Makala

KUTHUBUTU: Alijiuzulu kutoka GSU akazingatia sana muziki

November 9th, 2019 2 min read

Na PETER CHANGTOEK

TALANTA humsukuma mtu na huenda ikamfungulia milango.

Haya ni maneno yanayoendana zaidi na maisha ya msanii wa nyimbo za injili, Lucy Wangeci, ambaye alijitoa mhanga ili kukiendeleza kipawa chake cha uimbaji.

Msanii huyu anafichua kuwa alikigundua kipawa chake cha kuimba alipokuwa mtoto mdogo.

“Nilikuwa nikiimba nyimbo nilipokuwa shuleni, na kanisani,’’ anadokeza Wangeci.

Licha ya kipaji chake kudhihirika dhahiri shahiri alipokuwa mtoto, hakuurekodi wimbo wowote wakati huo, akijishughulika zaidi na masomo.

“Nilipokamilisha elimu yangu ya shule ya upili mwaka 2006, nilikaa mwaka mmoja, kabla sijaajiriwa katika kikosi cha polisi wa GSU. Nilipoajiriwa, nikahudumu katika Ikulu ya Rais, jijini Nairobi,’’ anasema Wangeci aliyewajibikia GSU kwa muda wa miaka sita.

Licha ya majukumu mengi kazini, msanii huyu alijifunga kibwebwe ili kuirekodi albamu yake ya kwanza.

Kwa hakika, juhudi zake za mchwa zilizaa matunda, maadamu alifanikiwa kuirekodi albamu ya kwanza mnamo mwaka 2008; mwaka mmoja tu baada ya kuajiriwa.

“Niliirekodi albamu yangu ya kwanza mnamo mwaka 2008, na yajulikana kama Umenitoa Mbali. Ina nyimbo saba,’’ anasema.

Baadhi ya nyimbo zilizomo katika albamu hii ni: Nimekukimbilia, Amka Tumsifu Bwana, Tukasimuliwa, Nitakusifu, Ukimwi, n.k.

Msanii huyu anasema kuwa, aliirekodi albamu ya pili, mwaka 2011, nayo yajulikana kwa jina Tusameheane Wakenya. Albamu hii ina nyimbo saba.

“Wimbo huu (Tusameheane Wakenya), ulichaguliwa na nikauimba kwenye maadhimisho ya Jamhuri, Desemba 12, 2011, yaliyoandaliwa katika Uwanja wa Nyayo. Nilikuwa nimeteuliwa kuwa mmoja wa wasanii wanaochipuka,’’ anasema Wangeci, ambaye hasa ni mzawa wa eneo la Mwea, Kaunti ya Kirinyaga.

“Wimbo huu ulimfurahisha sana Rais mstaafu, Mwai Kibaki,’’ aongeza Wangeci, ambaye alisomea Shule ya Msingi ya Mutithi, na hatimaye kujiunga na Shule ya Upili ya Wang’uru, kabla hajaajiriwa katika kikosi cha GSU.

Msanii huyu pia alijitahidi kwa jino na ukucha, ili kuirekodi albamu yake ya tatu. Aliudhihirisha umanju wake usiokuwa na kifani, alipoirekodi albamu ya tatu, Chineke, (Mungu), ambapo aliutumia mtindo wa Nigeria.

Mshika mbili moja humponyoka!

Mwimbaji huyu alishurutika kujiuzulu mwishoni mwa mwaka 2013, akiwa na dhamira ya kuiendeleza na kuikuza talanta yake.

“Nilikuwa nikialikwa katika sehemu mbalimbali kuongoaongoa. Nikaona kuwa kuliko kuomba idhini kila mara kazini ili kuenda kutumbuiza, ni afadhali niache kazi. Mwishoni mwa 2013 nikaacha kazi. Niliona ni kana kwamba nilikuwa nikilipwa pesa za serikali bure,’’ anasisitiza.

Ana albamu ya nne, Negukugocha (Nitakusifu) ambayo ina nyimbo saba.

Fauka ya hayo, anasema kuwa, ana albamu ya tano, ijulikanayo kwa jina Songa Mbele Kenya

Aidha, anasema kuwa, albamu zake tatu, zimerekodiwa kwa video tayari, na anaendelea kuzishughulikia nyingine zilizosalia. Kwa jumla, ana zaidi ya albamu tano.

Hakuna jambo lisilokuwa na changamoto. Baadhi ya changamoto ambazo msanii huyu amewahi kupitia ni ughushi wa muziki na tatizo la uuzaji wa nyimbo.

Hata hivyo, ananuia kuwaauni na kuwainua wasanii wanaochipuka katika siku za usoni, kwa kudura za Mwenyezi Mungu.