Habari za Kitaifa

Kutoboa masikio kulikuwa chanzo cha ndoa kusambaratika, mwanamke alia

January 30th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MHANDISI Susan Okeyo, alitengana na mumewe mwaka 2023, baada ya miaka 20, akisema penzi liliingia mdudu alipotoboa masikio na kuvalia vipuli ili kuongeza urembo.

Msukosuko wa ndoa ulipotokea, alikimbilia kwa ofisi za Wanasheria wa Kike (Fida) ili kumsaidia katika kesi ya kuomba talaka.

Bi Okeyo,39, ambaye ni mkazi wa Nairobi kwa sasa, alidai mumewe alitoka kwenye ziara ya kikazi, akapata ametoboa masikio na kuvalia vipuli.

“Wakati aliniuliza niliona ni mzaha kwa sababu aliniambia niondoke nyumbani kwa sababu hangeishi na mtu aliyetoboa masikio,” akadai Bi Okeyo.

Alidai kwamba alifukuzwa nyumbani mnamo Julai 2022.

Aliendelea kusimulia kwamba nyumba hiyo aliyofukuzwa, ilikuwa imejengwa katika kipande cha ardhi walichopewa na baba yake.

Miongoni mwa madai kwenye kesi iliyoko katika Mahakama ya Milimani ni kwamba hatimiliki ya ardhi ilibadilishwa bila idhini yake.

Alidai kwamba wakati wa kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Milimani, mumewe alikuwa ameanza mchakato huo katika katika mahakama ya Ngong.

“Wakili wangu alifahamishwa kuna kesi mahakama ya Ngong. Nilipofika mbele ya mahakama niliifahamisha kwamba sikuwahi kufahamishwa kuhusu mchakato wa kesi hiyo. Hakimu aliamuru kesi kufanyika jijini Nairobi,” akasema.

Mume ambaye ni mshtakiwa kwa kesi hiyo, akikana madai ya kumchapa aliyekuwa mke wake.

“Sikuwahi kumpiga mke wangu. Pili, sikufurahishwa na vipuli hivyo. Tulizungumza na nikamsihi kurejea nyumbani lakini alikataa,” akasema Bw E.O.K.

Utafiti wa 2023 uliofanywa na Shirika la Kitaifa la Takwimu Nchini (KNBS), unaonyesha visa vya talaka vimefikia asilimia 16, hii ikiwa na maana kwamba kati ya nyumba 18, nyumba moja ipo mbioni kutafuta talaka.