Habari Mseto

Kutoweka kwa vijana, kufufuka kwa MRC hofu kuu kwa usalama Pwani

December 23rd, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

TATIZO la ukosefu wa usalama liliendelea kusumbua wakazi wa ukanda wa pwani mwaka huu wa 2020. Baadhi ya matukio ya ukosefu wa usalama yatasalia kukumbukwa kwa siku nyingi zijazo ingawa kwa jumula visa vya utomvu wa usalama viliripotiwa kupungua.

Makundi ya vijana waliokuwa wakihangaisha wakazi yalizimwa kwa kiasi kikubwa mwaka huu na yaliyoripotiwa yalikabiliwa haraka.Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Al Shabaab, tukio la maafisa wa polisi kuwachapa wakazi wa Likoni, tishio la kufufuka kwa vuguvugu la MRC na kuendelea kutoweka kwa vijana.

Matukio hayo manne ni miongoni mwa yale ambayo yatasalia kwenye kumbukumbu za wakazi wa Pwani pamoja na wakuu wa usalama kutoka kanda hiyo.

Mwanzoni mwa mwaka huu magaidi wa Al Shabaab walivamia eneo la mafunzo ya kijeshi ya wanajeshi wa Amerika na wenzao wa Kenya eneo la Manda kaunti ya Lamu.

Shambulizi hilo la Januari tano lilipelekea kuuawa kwa raia watatu wa Amerika akiwemo mwanajeshi mmoja.Magaidi watano nao waliuawa wakati wa shambulizi hilo ambalo lilizua tumbo joto miongoni mwa wakuu wa usalama wa nchi hizo mbili.Wakazi walilazimika kuhama eneo la Manda wakihofia usalama wao.

Mwaka huu familia nyingi ziliendelea kulia kufuatia kutoweka kwa vijana.Hii imekuwa changamoto kuu ya kiusalama ambayo imewaacha wakazi kuendelea kuishi kwa hofu.

Ndani ya mwaka huu pekee, shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Africa lilisema kuwa limekusanya visa zaidi ya 20 vya watu kutoweka katika hali ya kutatanisha.

Visa hivi vimehusishwa na maafisa wa polisi ambao wamekanusha kuhusika kwao.Kaunti ya Kwale ndio imekuwa na idadi kubwa ya vijana walioripotiwa kutoweka.

Hali hiyo ya wasiwasi pia ingali miongoni mwa wakuu wa usalama baada ya madai ya kufufuka kwa kundi la Mombasa Republican Council (MRC).

Hii ni baada ya wanachama wa kundi hilo kukamatwa mwezi huu wa Disemba tarehe 2.Kufuatia kukamatwa kwa wanachama hao waziri wa usalama Fred Matiang’i alitangaza kuwa kikosi maalum kitatumwa eneo la Chonyi ili kudumisha usalama.

“Kuna wale ambao wanataka kuwalisha vijana wetu viapo ambavyo havieleweki ndio maana tunasema hatuwezi kubali hilo. Tutazidisha usalama eneo hili kwa sababu ya watu wetu,” akasema Dkt Matiang’i alipozuru Pwani mwezi huu.