Habari

Kutumia kondomu kukinga simu ni hatari, wavuvi waonywa

September 11th, 2018 2 min read

Na WINNIE ATIENO

WATAALAMU wa kiafya Mombasa Jumanne walionya wavuvi dhidi ya kutumia mipira ya kondomu kuzuia simu zao kuingia maji wanapozama baharini katika shughuli za uvuvi katika Bahari Hindi.

Aidha wavuvi hao huanza kwa kuosha au kupanguza kondomu hizo ili kuondoa mafuta kisha wanaingiza simu zao na kufunga fungo kila wanapoenda kuvua.

Wanapozama huwa wanatoa simu zao na kupiga kwa wenzao waende wawaokoe.

Juli tarehe 9, wavuvi wanne walipotea baharini na wengine wawili kuokolewa baada ya boti lao kuzama katika bahari hindi huko Mombasa.

“Ni mpira wa kondomu ambayo ilituokoa, ilikuwa saa tano za usiku ambapo boti letu lilizama tukawapigia wenzetu kwa kutumia simu ambayo tulikuwa tumeivisha kondomu. Boti ilikuja kutuokoa lakini sababu ilikuwa haina taa alishindwa kutupata,” akasema Bw Jaffary.

Mshauri wa nyanjani Karisa David ambaye amepeana huduma za HIV kwa zaidi ya makundi 14 ya uvuvi huko Mombasa alionya dhidi ya matumizi mabovu ya kondomu. “Inatumiwa kujikinga dhidi ya magonjwa ya zinaa wala si kwa simu. Mipira ambayo ni raba ni hatari kwenye mazingira ya bahari hata kwa samaki,” akaonya.

Alisema ni changamoto na itabidi wakabiliane nayo kwa kuwapa nasaha wavuvi hao.

Baraza la kitaifa la kudhibiti maambukizi ya ukimwi (NACC) nao walitoa ilani kwa utumizi mbovu wa kondomu.

Mshirikishi wa baraza hilo, Julius Koome alisema hulka hiyo inafaa kukomeshwa kupitia mdahalo.

Lakini wavuvi hao walisema watabadilisha endapo watapewa njia mbadala ya kuwaokoa kwenye hatari baharini.

Mei tarehe 11, Jaffary na wenzake wanne walienda kuvua eneo la Shelly Beach ambapo boti yao ilizama baada ya kusombwa na mawimbi makali.

“Tuliogelea kwa dakika chache kabla ya mwenzetu ambaye alikuwa amevisha simu kondomu kupiga simu na tukaja kuokolewa. Hii ni baadhi ya mikasa ambayo ilitupa moyo zaidi kuendelea kutumia mipira ya kondomu kwenye shughuli zetu,” akasema.

Kwenye mahojiano huko Nyali Beach, wavuvi hao walisema wakiongozwa na Bw Ali Kibwana ambaye ametumia mbinu hiyo kwa karibu mwaka mzima sasa.

Huwa anachukua kondomu hizo zinazopeanwa bure na serikali katika vituo vya afya huko Mombasa.

Kwa siku wavuvi 50 hutumia kondomu 50 ‘kuokoa’ simu zao ili zisiharibike kwenye maji wanapovua.

“Tungekuwa na njia mbadala tungetumia, maanake tunakabiliana na unyanyapaa sababu ya matumizi ya kondomu wengi wakidhania sisi ni washerati lakini hatuna budi,” akasema.

Mvuvi huyo ambaye amvua kwa zaidi ya miaka 10 alisema mpira wa kondomu huwasaidia wakati bahari inapochafuka na kunakuw ana mawimbi makali inayoangusha boti zao na wanazama.

Alisema kama si kodomu wangekuwa wameshakufa maji walipozama.