Kimataifa

Kuvuta bangi yenye sumu ya chura hunituliza nisifanye unyama – Mike Tyson

May 21st, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

ALIYEKUWA mwanabondia maarufu duniani Mike Tyson ametoboa kuwa kuvuta bangi iliyo na sumu ya chura ndiko kumekuwa kukimtuliza kutokana na tabia ya kupatwa na hasira ama mawazo ya kufanya vitendo haramu.

Tyson, ambaye alikuwa mmoja kati ya wanabondia walioogopwa sana duniani katika historia ya uanabondia kutokana na jinsi alivyopigana amekuwa na matatizo tangu alipoacha kazi hiyo.

Mbeleni amehudumu kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kumnajisi msichana tineja, mnamo 1991. Alikuwa amefungwa miaka sita.

Tyson ambaye ni balozi wa bangi, hata hivyo, sasa anasema kuwa hataki kuonekana kama mnyama jinsi alionekana mbeleni, akisema kuvuta bangi yenye sumu hiyo, ambayo hupatikana katika jangwa la Sonoran, Mexico kumemsaidia kupunguza hasira.

“Sitaki kufa nikiwa na unyama kiasi hicho, sitaki kukumbukwa kama mtu wa aina hiyo,” akasema Tyson, mwenye umri wa miaka 52 sasa.

Alisema mbeleni alikuwa ameingiwa na hali mbaya, ambayo ilimfanya kuwa na tabia zisizo za kupendeza.