DOUGLAS MUTUA: Kuwaadhibu wakuu wa magereza ni danganya-toto ya kuficha aibu

DOUGLAS MUTUA: Kuwaadhibu wakuu wa magereza ni danganya-toto ya kuficha aibu

Na DOUGLAS MUTUA

USIDANGANYIKE! Serikali imewafuta kazi na kuwakamata wakuu wa magereza ili kuwapumbaza Wakenya na ulimwengu kwa jumla eti vita dhidi ya ugaidi vimepamba moto.

Uongo! Hiyo, amini usiamini, ni danganya-toto inayonuiwa kuficha fedheha na ithibati ya usimamizi mbaya wa usalama nchini.

Kutoroka jela kwa magaidi watatu hatari, miongoni mwao aliyepanga mauaji ya wanafunzi 148 wa Chuo Kikuu cha Garissa, ndiko kulisababisha wakuu wa magereza watimuliwe.

Kumbuka, ni lazima washirika wetu katika vita dhidi ya ugaidi wasadikishwe kwamba mafedha yao yanatenda kazi, hatuchezi na waovu wanaoshirikiana na magaidi.

Haikosi aliyekuwa kamishna mkuu wa magereza, Bw Wycliffe Ogallo, alishtuka alipoviziwa na kukamatwa na maafisa wa polisi wa kupambana na ugaidi (ATPU).

Huo ulikuwa mshtuko wa pili kwa kuwa muda mfupi awali, alikuwa amepigwa kalamu na Rais Uhuru Kenyatta akamteua Brigedia John Kibaso Warioba kuchukua nafasi yake.

Nasema alishtuka kwa sababu, labda katika fikra zake, hakuwahi kutafakari akiwa mteja wa vikosi vya usalama kwani amekuwa mmoja wavyo, tena akiwapokea wahalifu sugu kuwafunza nidhamu.

Katika utumishi wa umma Kenya, yapo matatizo ambayo kamwe hayatarajiwi kuwakumba watu wa vyeo vya juu kama Bw Ogallo.

Hata mkuu wa gereza la Kamiti, Bw Charles Mutembei, hakutarajia siku yake iishe vibaya kwani amezoea kubweka amri na kusujudiwa na wadogo wake pamoja na wafungwa.

Kutiwa mbaroni kwa askari jela kadha kuhusiana na kisa hicho cha watoro hatari lazima kulikuwa kumempa utulivu wa moyo asidhani yeye pia na mdogo wake wangekamatwa.

Wasichokitambua maafisa hao watatu ni kwamba, kashfa iliyoikumba idara yao ilikwisha fikia kiwango cha kimataifa, hivyo lazima kafara itolewe na wao ndio kondoo hasa!

Nasisitiza hatua ya kuwafuta kazi na kuwakamata ilichukuliwa ili jamii ya kimataifa ifurahishwe mpaka ipumbazike; si mara ya kwanza kwa mahabusu kutoroka.

Nilipokuwa ripota wa mahakamani, yapata mwongo mmoja uliopita, watuhumiwa walikuwa wakitoroka mara kwa mara wakiletwa mahakamani au kurejeshwa jela.

Visa hivyo vilikuwa vingi hivi kwamba, kwa kiasi fulani, vilizoeleka. Askari jela waliotorokwa wafungwa wakichukuliwa hatua za kinidhamu tu lakini hawakufutwa kazi wala kushtakiwa.

Hata katika vituo vya polisi kote nchini, ni kawaida kwa watuhumiwa hatari kuachiwa huru badala ya kupelekwa mahakamani.

Aliyeshtaki hubaki kinywa wazi asiwe na la kufanya.

Je, unakumbuka kisa ambapo magaidi waliokuwa njiani kuelekea Nairobi huku wakibeba silaha nzito-nzito waliwahonga polisi kwenye kizuizi cha barabarani na wakaruhusiwa kupita?

Ripoti kadha zinaonyesha kwamba polisi, askari magereza na hata wanajeshi wa Kenya wako radhi kuhatarisha usalama wetu sote mradi wanapata fedha.

Kwa tamaa ya pesa na wepesi wa kushawishika, maafisa wa usalama wa Kenya wanaweza tu kufananishwa na makahaba wanaozurura mitaani usiku wakifanya biashara isiyohitaji mtaji.

Hiyo si siri. Hata Rais Uhuru Kenyatta anajua. Na hajafanya chochote kubadili hali hiyo kwa miaka tisa ambayo ameiongoza nchi, hivyo kuwafuta kazi wakuu wa magereza hakufai.

Ikiwa kuwafuta kazi wanaosimamia idara ambazo zinazembea ndiko suluhisho, basi itabidi Rais Kenyatta mwenyewe ajiuzulu kwani ni mmoja wao.

Kisa na maana ni kwamba, kwa muda wa miaka tisa, amekuwa akidai atapambana na ufisadi, ambao kwa hakika ni tishio kwa usalama wa nchi, lakini wapi!

Ukiangalia ugaidi ulivyosambaa kote Afrika wakati huu, kisha ukumbuke Uganda imeshambuliwa hivi majuzi, unasalitika kuiombea nchi ipate viongozi bora, si bora viongozi tu.

mutua_muema@yahoo.com 

  • Tags

You can share this post!

Mamilioni ya Ruto yawasha moto sehemu tofauti nchini

WANDERI KAMAU: Wanasiasa wakuu nchini wana...

T L