MALEZI KIDIJITALI: Je, kuwapa watoto uhuru ni kuwaharibu?

MALEZI KIDIJITALI: Je, kuwapa watoto uhuru ni kuwaharibu?

Na BENSON MATHEKA

KASUNI na mkewe Ivy wamelaumiwa na wazazi wenzao kwa kuwapa watoto wao wawili uhuru wa kufanya watakalo.

Baadhi wanadai kwamba wawili hao wamewatelekeza watoto hao jambo ambalo Ivy anakanusha.

“Tunachofanya kama wazazi ni kuwafunza watoto wetu uhuru wao ili wabaini kuchagua mazuri na mabaya. Tunawaruhusu kucheza na watoto wengine tofauti na majirani wanaowafungia watoto wao ndani ya nyumba watazame runinga na kushiriki michezo mtandaoni. Wakiwa nje, tunahakikisha wako salama na baadaye tunaketi nao watueleze walichojifunza na athari zake kwa maisha yao,” asema Ivy.

Wataalamu wa malezi wanakubaliana na Ivy kwamba watoto wanafaa kupatiwa uhuru na kufunzwa jinsi ya kujiamulia mambo.

“Kumfungia mtoto na kumsimamia kila wakati ukimuelekeza la kufanya hakufai. Mpe uhuru ajifunze mambo mapya huku ukimshauri kuepuka yaliyo mabaya,” asema Sydney Ooko, mtaalamu wa malezi katika kituo cha Liberty Intensity mjini Athi River.

“Kusaidia watoto vyema ni kuwafunza kujiamulia mambo. Kama mzazi, utakuwa ukijiweka katika hali nzuri sana ya kujua una watoto wanaoweza kufanya maamuzi yanayofaa na kuepuka hatari inapowakabili,” asema.

Dkt Erick Levya, mwanasaikojia anayehusika na maslahi ya watoto anasema kwamba ni muhimu kuwapa watoto uhuru wa kujifunza mambo yanayowavutia.

“Ukisimamia mtoto kama nyapara, unamnyima fursa ya kukuza akili yake. Ukimfungia ndani ya nyumba, unamwekea mipaka ya kufikiria tofauti na anapokuwa nje akiwa na wenzake,” asema.

Dkt Levya anasema lengo la kuwapa watoto uhuru kiasi ni kuwawezesha kujiamulia wenyewe ikiwemo jinsi ya kuepuka kushawishiwa na wahalifu wakiwemo walanguzi wa watoto.

“Ni tofauti na kuwatelekeza watoto. Usiwalinde kupita kiasi lakini wafunze kuepuka hatari na wasiende mbali na nyumbani. Lazima uwaonyeshe kwamba unawaamini na uwafunze kujiamini. Pia inawapa wazazi muda wa kuwa peke yao ndani ya nyumba,” aeleza.

You can share this post!

Man-United wamfuta kazi kocha Ole Gunnar Solskjaer

BAHARI YA MAPENZI: Ukatili wa kijinsia ni suala la kimamlaka

T L