Michezo

KUWENI NA SUBIRA: Ole Gunnar Solskjaer aomba muda kuimarisha Manchester United

October 9th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United amesema anahitaji muda kuirejesha klabu hiyo katika ubora wake.

Raia huyo wa Norway alisema hayo kutokana na presha inayomkabili baada ya vijana wake kulazwa 1-0 na Newcastle United, mwishoni mwa wiki.

Matokeo hayo yamekuja siku chache tu baada ya sare ya kutofungana na AZ Alkamaar ya Uholanzi katika pambano la Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya.

Lakini kocha huyo amewataka mashabiki wa mabingwa hao wa zamani kuwa wavumilivu, wakati akiendelea kujenga kikosi cha kutisha siku za usoni.

Solskajaer alisema mashabiki hawafai kutarajia matokeo ya haraka kwa sababu kikosi chake hakijakamilika, huku akiwataka wawe na subira.

Alisema, ili warejee kwenye mafanikio waliyokuwa nayo miaka ya 1990, sharti kikosi kijengwe kupitia kwa wachezaji wa sasa ambao wengi ni chipukizi.

Solskajer ni kocha wa nne tangu Alex Ferguson astaafu, lakini hakuna mafanikio yoyote ambayo yamepatikana, bali inazidi tu kushuka.

“Tuko katika kipindi tofauti ambacho tunahitaji uvumilivu wa kutosha ili tujenge timu mpya. Mashabiki wanafaa kukumbuka kwamba malengo yetu bado hai. Nipo tayari kuirudisha Manchester katika ubora wake, lakini lazima tuweke misingi mizuri ili timu iwe na makali ya awali.

“Timu itarejea kwenye utamaduni wake wa zamani baada ya makinda hawa kupata uzoefu wa kutosha, hivyo wanahitaji muda wa kutosha kukamilika.

“Sharti mashabiki waelewe kwamba hata mimi na benchi langu la ukufunzi husononeka wakati tunaposhindwa, lakini tunaelewa lazima baadhi ya wachezaji wapewe muda wa kutosha,” aliongeza.

Manchester ambao hawana rekodi nzuri ya mechi za ugenini, haijashinda mechi 10 baada ya kushindwa saba na kutoka sare mara nne.

Manchester wanakamata nafasi ya 12 jedwalini, kwa pointi tisa kutokana na mechi nane, na hawajafunga zaidi ya goli moja tangu waanze msimu kwa ushindi mkubwa wa 4-0 dhidi ya Chelsea. Kufikia sasa, wako tu pointi mbili juu ya msitari wa shoka la timu kushuka.

Kukwaana na Liverpool

Mechi yao ijayo itakuwa dhidi ya Liverpool ambao wanahitaji tu ushindi na kuifikia rekodi ya Manchester City ya kushinda mechi 18 za EPL mfululizo.

Matokeo haya yanatokea baada ya naibu Afisa Mkuu wa klabu hiyo, Ed Woodward kuwataka mashabiki waendelee kutulia wakati kocha anafanya kila jambo kuhakikisha timu hiyo imerejea katika ubora wake wa miaka ya awali.

Solskjaer alipewa mamlaka ya kuwa kocha mkuu mnamo Machi 28 kujaza nafasi ya Jose Mourinho aliyetimuliwa mapema mwaka huu.

Alifanikiwa kupata ujira huo baada ya kushindwa mara moja pekee kati ya mechi 17 alizoongoza kama kocha wa muda, matokeo ambayo ni asilimia 85.35.