Kuzimwa kwa BBI kulivyovuruga siasa za urithi 2022

Kuzimwa kwa BBI kulivyovuruga siasa za urithi 2022

Na BENSON MATHEKA

Kuzimwa kwa mchakato wa kubadilisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), kumevuruga mipango ya wanasiasa walionuia kutumia marekebisho hayo kufufua maisha yao ya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mahakama ya Rufaa iligonga msumari wa mwisho kwenye jeneza la BBI kwa kukubali uamuzi wa majaji watano wa Mahakama Kuu waliosema mchakato huo haukuwa wa kikatiba.

Wanasheria na wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba uamuzi huo uliojiri chini ya mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ujao, sio tu pigo kwa waanzilishi wa Mpango wa Maridhiano nchini, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, mbali umezika matumaini ya vigogo wa kisiasa waliokuwa wakiutengemea kusuka miungano ya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa umevuruga kwa kiwango kikubwa mipango ya wanasiasa kusuka miungano kabla na hata baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.Wengi ambao wamekuwa kwenye baridi ya kisiasa kwa miaka mingi walitarajia kuitumia kufufua maisha yao ya kisiasa lakini mikakati yao imetibuka,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Hasa anasema kuwa uamuzi huo umeathiri mikakati ya Rais Kenyatta kupanga siasa za urithi wake. “Rais yuko mbioni kupanga urithi wake na alitarajia kutumia marekebisho ya katiba kubuni kikosi cha kumkabili Naibu Rais William Ruto ambaye walitofautiana kufuatia handisheki yake na Bw Odinga. Kuna vigogo wa kisiasa wa maeneo tofauti ambao amekuwa akijaribu kuwaunganisha wamkabili Dkt Ruto na alitengemea nyadhifa ambazo BBI ingebuni,” asema Bw Kamwanah.

BBI ilipendekeza kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu, manaibu wawili, mawaziri kuwa wabunge na kiongozi rasmi wa upinzani.

Wadadisi wanasema viongozi wanaomezea mate urais na ambao walikuwa wakitegemea marekebisho hayo kujipanga wamevurugwa.

Miongoni mwao ni kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC), Moses Wetangula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu.

Wanne hao wamekuwa wakisuka muungano wa One Kenya Alliance (OKA). Rais Kenyatta amekuwa akiwakutanisha na Bw Odinga akiwarai washirikiane naye kwenye uchaguzi mkuu ujao ili kumbwaga Dkt Ruto.

Vyama vya ODM na Jubilee pia vinaendeleza mazungumzo kwa lengo la kuungana kwenye uchaguzi mkuu ujao na inasemekana vimeshawishi vyama kadhaa viidogo kushirikiana navyo.

Wadadisi wanasema kwamba baadhi ya washirika wa vigogo hao waliokuwa wakiunga BBI wakimezea mate nyadhifa za mawaziri, watalazimika kujipanga upya.

“BBI ilikuwa imewapa matumaini makubwa wanasiasa wengi kuanzia madiwani walioshawishiwa kuiunga, wanaomezea mate ubunge na urais. Itabidi waanze mikakati yao upya,” asema mchanganuzi wa siasa Leonard Ochuka.

Mdadisi huyu asema kuzimwa kwa mchakato huo kumeathiri kabisa siasa za urithi ambazo Rais Kenyatta alikuwa amesuka.

“Lakini ninaamini alikuwa ameweka mikakati mbadala ambayo itaibuka wakati wowote kuanzia sasa. Lililo bayana ni kuwa kutakuwa na mabadiliko makubwa katika siasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Ushirika wa kisiasa uliokitwa kwenye BBI utasambaratika kila mwanasiasa akijaribu kuokoa maisha yake ya kisiasa,” asema Ochuka.

Ingawa baadhi ya vigogo wa kisiasa waliounga BBI walisema kwamba wataheshimu uamuzi wa Mahakama, Ochuka anasema ni mbinu ya kuepuka kusutwa na umma.

“Ulikuwa mchakato wa kulazimisha kwa lengo la kupanga urithi 2022 lakini haukuhusu maslahi ya wananchi wa kawaida. Pigo kubwa ni kwa Rais Kenyatta na mshirika wake katika handisheki Raila Odinga. Naona handisheki ikitikisika kwa kiwango fulani,” asema.

Mwaka jana, Bw Odinga alinukuliwa akisema handisheki yake na Rais Kenyatta ingeisha baada ya Katiba kurekebishwa. Hata hivyo, iliibuka kuwa, Rais Kenyatta anataka waziri mkuu huyo wa zamani kuwa mrithi wake kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Kulingana na Bw Odinga, amesonga mbele na mipango yake ya kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao bila BBI na tayari amezindua kampeni ya Azimio la Umoja analolenga kuleta pamoja viongozi wa maeneo tofauti kuunga azima yake ya kugombea urais kwa mara ya tano.

Kulingana na Kamwanah, Naibu Rais William Ruto, ambaye alichangamkia uamuzi wa Mahakama ya Rufaa alivyofanya Mahakama ya Juu ilipozima BBI, anatarajia kunufaika zaidi iwapo vinara wanaosuka muungano wa OKA hawatakubali kuungana na Bw Odinga.

Wiki jana, Dkt Ruto alisema kuna wanasiasa wengi wanaomuunga mkono lakini wanaogopa kuhangaishwa na maafisa wa serikali wakijitokeza wakati huu.

Duru zinasema kwamba Rais Kenyatta hajachoka kujaribu kupatanisha vinara wa OKA na Bw Odinga, na amepanga mkutano mwingine kujadili mstakabali wa mikakati ya siasa za urithi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Mkutano huo utakaokuwa wa tatu ndani ya mwezi mmoja, utajadili njia mbadala za kurekebisha baada ya BBI kushindwa ikiwemo uwezekano wa kutumia bunge kufanikisha baadhi ya mapendekezo katika BBI.

You can share this post!

Rais Uhuru abadilisha mbinu kuendelea kung’ata Mlimani

Mwanamume na wanafunzi wawili waangamia kisimani