Kuzimwa kwa Reggae pigo kwa Ruto licha ya kusherehekea

Kuzimwa kwa Reggae pigo kwa Ruto licha ya kusherehekea

Na LEONARD ONYANGO

HATUA ya Mahakama Kuu kutupilia mbali Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) ni pigo kwa Naibu wa Rais William Ruto licha ya kusherehekea uamuzi huo.

Endapo BBI ingepitishwa na Wakenya, wadadisi wanasema, Dkt Ruto angetumia nyadhifa za ziada zilizomo katika mswada huo kuvutia vigogo kutoka maeneo yanayochukuliwa kuwa ngome za Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Kwa mfano, Dkt Ruto angetoa wadhifa wa naibu rais kwa watu kutoka eneo la Mlima Kenya, uwaziri mkuu kwa viongozi wa Magharibi, manaibu waziri mkuu kutoka Nyanza na Pwani,” anasema Bw Mark Bichachi, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Mswada wa BBI unapendekeza kupanuliwa kwa serikali kwa kuongeza nyadhifa zaidi kama vile nafasi ya waziri mkuu atakayekuwa na manaibu wawili.

Mswada huo pia unapendekeza kuwa mawaziri wawe wakiteuliwa kutoka Bungeni – kumaanisha kwamba wandani wake wengi wangenufaika iwapo Dkt Ruto atachaguliwa kuwa rais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Naibu wa Rais Ruto hajakuwa na msimamo thabiti kuhusu BBI – amekuwa akipinga na kisha kuunga mkono.Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Herman Manyora ambaye ni mdadisi wa masuala ya kisiasa, anasema kuwa hatua ya Dkt Ruto kukosa msimamo, ilisababisha wabunge na maseneta wanaomuunga mkono kugawanyika wakati wa kupigia kura mswada huo katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Baadhi ya wabunge na maseneta wanaounga mkono Dkt Ruto, maarufu Tangatanga, waliounga mkono mswada wa BBI Bungeni ni David Sankok (Maalumu) Kareke Mbiuki (Maara), Joash Nyamoko (Mugirango Kaskazini ),William Chepkut (Ainabkoi), Purity Kathambi (Njoro), David Gikaria (Nakuru Mashariki), Gideon Koske (Chepalungu).

Bw Manyora, hata hivyo, anasema kuwa Bw Ruto huenda akatumia uamuzi huo wa Mahakama Kuu kujiongezea umaarufu wa kisiasa na kuwaponda wapinzani wake wakuu ambao ni Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali BBI Alhamisi jioni; Dkt Ruto pamoja na wandani wake, walisherekea huku wakimshukuru Mungu.

You can share this post!

Karua na kundi la Tangatanga walivyoungana kushambulia BBI

ODM wadai Matiang’i anatumia polisi kuwahangaisha Kisii