Makala

KWA KIFUPI: Asali ni dawa ya kikohozi – Utafiti

August 25th, 2020 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

IKIWA unasumbuliwa na kikohozi, mafua au kufungana kwa koo na pua, unaweza kujaribu kutumia asali.

Watafiti wa Chuo Kikuu cha Oxford kupitia ripoti yao iliyochapishwa katika jarida la BMJ Evidence Based Medicine, wanasema kuwa asali inatibu kikohozi na kufungana kwa pua na koo kwa haraka zaidi kuliko dawa zilizopo hospitalini.

Watafiti hao sasa wanataka madaktari washauri wagonjwa wao kutumia asali badala ya dawa za kawaida zinazouzwa madukani.

Kwa muda mrefu wazazi wamekuwa wakitumia asali kutibu kikohozi na mafua miongoni mwa watoto. Lakini hakukuwa na ushahidi kwamba asali pia inaweza kuwasaidia watu wazima.

Watafiti hao walisema kuwa asali inaweza kuponya kikohozi ndani ya siku tatu.

Wanasayansi hao, hata hivyo, wanasema kuwa mimea ambayo hutumiwa na nyuki kutengeneza asali hubadilika kutoka eneo moja hadi nyingine.

“Hivyo, kuna uwezekano wa kutumia asali na isikufae,” inasema ripoti ya watafiti hao.

Inaongeza: “Hata hivyo, tunawashauri madaktari kuwaeleza wagonjwa wao kutumia asali kwani inapatikana kwa urahisi na inauzwa kwa bei nafuu.”