Makala

KWA KIFUPI: Dawa ya kuzuia damu kuvuja bila kuganda sasa imepatikana

September 10th, 2019 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

IKIWA wewe ni mmoja wa watu ambao damu huvuja kwa muda mrefu bila kuganda unapojikwaa, basi kuna habari njema kwako.

Ugonjwa wa kuvuja damu bila kukoma hujulikana kama Haemophilia A.

Wanaouvuja damu kwa muda mrefu wanapofanyiwa upasuaji, hutokwa damu kwenye fizi mara kwa mara.

Tatizo hilo huwa changamoto kubwa kwa watoto kwani wanajikata mara kwa mara wanapochezea vitu vyenye ncha kali kama vile wembe, kisu, panga na kadhalika.

Wagonjwa wa Haemophilia A, hawana aina fulani ya protini ambayo husababisha damu kuganda au ‘kidonda kukauka’.

Waathiriwa hulazimika kutumia dawa inayofahamika kama prophylaxis inayowezesha damu kuganda. Dawa hiyo hutumiwa kila baada ya wiki chache.

Lakini wizara ya Afya nchini Uingereza imeidhinisha dawa mpya inayojulikana kama Hemlibra inayomwondolea mwathiriwa usumbufu wa kwenda hospitalini kila baada ya wiki chache kutafuta dawa ya kugandisha damu.

Dawa hiyo mpya huwekwa chini ya ngozi kwa kutumia sindano.

Maradhi hayo hurithishwa kutoka kwa wazazi hadi kwa mtoto na huathiri zaidi watoto wa kiume.