Makala

KWA KIFUPI: Maradhi ya ngozi yanayosababisha mwasho, ukavu na vipele vyekundu

September 3rd, 2019 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

UKURUTU au ukipenda Eczema ni hali ambapo sehemu za ngozi huanza kuasha, kubadilika rangi na kuwa nyekundu, vile vile kukwaruzika. Wakati mwingine huenda malengelenge au vipele vikatokea.

Kuna aina mbalimbali za ukurutu ikiwa ni pamoja na:

• Allergic contact dermatitis: Hii hutokana na mgusano wa ngozi na kitu au kichochezi ambacho kwa sababu ya mzio (allergy) kinasababisha mwasho.

•  Dyshidrotic eczema: Hii husababisha mwasho kwenye viganja vya mkono na nyayo za mguu na mara nyingi husababisha malengelenge au vipele.

• Neurodermatitis: Hii husababisha kuonekana kana kwamba ngozi inaota magamba kwenye kichwa, miguu, kifundo cha mkono, na sehemu ya chini ya miguu. Hasa husababishwa na mwasho kutokana na mng’ato wa mdudu.

•  Nummular eczema: Sehemu za ngozi iliyo na mwasho huwa ngumu na kuonekana kana kwamba ina magamba huku ikisababisha mwasho.

• Seborrheic eczema: Hii husababisha ngozi kuwa na mafuta na kubadili rangi na kuwa manjano hasa kwenye ngozi ya kichwa na usoni.

• Stasis dermatitis: Mwasho wa ngozi hasa katika sehemu ya chini ya mguu, hali ambayo husababishwa na matatizo ya mzunguko wa damu.

Chanzo

Kuna baadhi ya vyakula ambavyo huchochea dalili za hali hii kama vile njugu na vyakula vya bidhaa za maziwa. Aidha, ishara za hali hii zaweza kuchochewa na masuala ya kimazingira kama vile moshi na chavua. Mara nyingi ishara hutofautiana na umri, lakini kwa kawaida ishara hufanana.

Dalili

Kwa kawaida ukurutu waweza kusababisha upele mkavu na unaowasha, lakini mara nyingi ishara hutofautiana kulingana na umri wa mhusika. Watoto wengi hukumbwa na hali hii kabla ya kuhitimu miaka mitano.

Nusu ya walioathirika, huendelea kukumbwa na hali hii hata katika umri wa utu uzima.

Dalili kwa watoto chini ya miaka miwili

• Upele hasa kwenye ngozi ya kichwa na mashavu

• Kwa kawaida upele huu huvimba kabla ya kuanza kuvuja

• Upele huu waweza kusababisha mwasho ambapo mara nyingi huathiri usingizi

Dalili kwa watoto kati ya miaka miwili na umri wa kubalehe

• Upele kwenye mikunjo ya viwiko au magoti, shingo, kifundo cha mkono na mguu, na mkunjo kati ya makalio na miguu.

• Upele unavimba na huenda ukabadili rangi na kuwa nyeupe au nyeusi.

• Upele huu waweza kujazana, hali inayofahamika kama ‘lichenification’.

Dalili miongoni mwa watu wazima

• Upele kwenye mkunjo wa viwiko na ukosi wa shingo

• Upele unafunika sehemu kubwa ya shingo

• Upele unaongezeka kwenye ngozi, uso na sehemu inayozingira macho

• Upele unaanza kusababisha ngozi kukauka na kuasha sana na hata kusababisha maambukizi

Kuzidi kujikuna na kugusa sehemu zilizoathirika kwaweza kusababisha mambukizi ya ngozi.

Tiba

Japo hali hii haina tiba, kuna mbinu zinazosaidia kukabiliana nayo kama vile kupaka mafuta katika sehemu ya ngozi iliyoathirika. Aidha, kuna baadhi ya watu jinsi wanavyoendelea kukua kiumri, tatizo hili hutokomea. Tiba huhusisha kutibu ngozi iliyoathirika na kukabiliana na dalili.

Mbinu za kinyumbani za kukabiliana na makali

• Kuoga kwa maji yaliyopashwa moto

• Kujipaka mafuta katika kipindi cha dakika tatu baada ya kuoga ili kufungia unyevu kwenye ngozi

• Kujipaka mafuta kila siku

• Kuvalia mavazi yaliyoundwa kwa kitambaa cha pamba au vitambaa vyepesi huku ukiepuka vile vigumu, na pia nguo zinazobana

• Kutumia sabuni na mafuta yasiyo na harufu kali

• Kujipangusa kwa utaratibu baada ya kuoga

• Kuepukana na vichocheo vinavyosababisha ukurutu

• Dumisha kucha fupi za mkononi ili kuzuia ngozi kuchubuka unapojikuna