• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Mvinyo, juisi na jemu ya mtama kutoka JKUAT

Mvinyo, juisi na jemu ya mtama kutoka JKUAT

NA SAMMY WAWERU

MTAMA ni mojawapo ya mazao wanayohimizwa wakazi wa maeneo kame kukuza kukabili baa la njaa na kujiendeleza kimaisha.

Huku kaunti 24 zikikabiliwa na kero ya ukame kufuatia kukithiri kwa kiangazi, zao hilo litawasaidia kimapato na kimaendeleo.

Athari za mabadiliko ya tabianchi, zimechangia kubadilika kwa hali ya anga nchini misimu ya mvua ikikawia.

Mtama unastahimili makali ya kiangazi, uvumbuzi wa mbegu za kisasa kupitia tafiti za wanasayansi katika utandawazi wa kilimo ukisaidia zao hilo kuhimili mkumbo wa magonjwa ibuka.

Baada ya mavuno ya mtama, wengi hulisha mifugo mabua yake na wengine kuiacha kuozea shambani.

Ulijua mabua hayo yanaweza kugeuzwa mapato? Winnie Nyonje ni msomi na mtafiti wa kilimomseto.

Anasema utafiti umeonyesha kuwa juisi ya mtama inaweza kuongezwa thamani kuunda mvinyo.

Maarufu kama “miwa” ya jangwani, juisi hii ina kiwango cha juu cha sukari.

“Kupitia tafiti kadha za Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), imebainika kuwa mabua ya mtama yanaweza kuunda juisi ya kunywa na mvinyo,” anaeleza.

Mabua hao hukatwa baada ya nafaka kuvunwa shambani.

“Ivunwe nafaka ikiwa imekomaa na mabua yawe rangi ya kijani,” asisitiza Nyonje.

Katika awamu hiyo mabua yana kiwango cha juu cha juisi. Majani yanaondolewa na mabua hayo kuoshwa. Kwa kutumia mashine aina ya roller cane extractor au stalk crusher, rina juisi.

“Kiwango cha juisi kinategemea awamu ya mavuno na utunzi wa mtama,” adokeza mtafiti huyo aliye na Shahada ya Digrii katika Sayansi ya Kilimomseto na Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Chakula na Afya.

Hatua inayofuata ni kugeuza juisi iwe chachu ili kupata mvinyo.

Kulingana na mtafiti huyo, kiwango cha juu cha sukari katika mabua ya mtama pamoja na madini ya nitrojini, husaidia hamira kumea na hivyo juisi kuwa chachu. Mchakato huu huchukua siku 21.

Chini ya miradi kadha inayoongozwa na Profesa Willis Owino katika chuo hicho cha JKUAT, mvinyo huo unaweza kusindikwa kwa kutumia matikiti maji, mananasi na zabibu.

“Mvinyo wa juisi ya mtama una asilimia 12 ya kiwango cha pombe,” Prof. Owino anadokeza.

Sharubati husindikwa kwa juisi ya mananasi na machungwa. Bidhaa nyingine zinazotengenezwa kutokana na juisi ya mtama ni jemu, shira na mamaledi.

Mtafiti Winnie Nyonje na Prof. Willis Owino kutoka JKUAT, wakionyesha bidhaa zilizoundwa kwa kutumia juisi ya miwa ya mtama. PICHA | SAMMY WAWERU

Ingawa bidhaa hizo hazijaingia sokoni rasmi, juisi hupakiwa katika vipimo vya mililita 500 huku jemu, mamaledi na shira zikiwa gramu 500. Mvinyo hutiwa katika vichupa vya mililita 750.

“Tunasubiri Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs), kutupa kibali kwa sababu haijaunda viwango vya ubora kwa bidhaa za mtama zilizoongezwa thamani,” Nyonje aeleza Akilimali.

Mwanasayansi huyo alikuwa miongoni mwa watafiti na wakulima wa mazao ya maeneo kame, waliopata fursa ya kuonyesha bidhaa zao wakati wa maonyesho ya The International Crops Research Institute for the Semi-Arid Tropics (ICRISAT), jijini Nairobi majuzi.

Shirika hilo huendesha miradi ya kuinua wakulima katika maeneo kame, na linaadhimisha miaka 50 katika uvumbuzi wa bunivu za Kisayansi kuboresha kilimo tangu lianzishwe 1972.

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Kisiagi cha kuongeza thamani ya uyoga

Gavana ashauri wakazi kutumia vyema mikopo

T L