Makala

KWA KIFUPI: Sugua meno yako mara kwa mara ujiepushe na maradhi ya ubongo

August 13th, 2019 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

WENGI husugua meno ili kuepuka kutoa pumzi yenye harufu mbaya.

Lakini sasa wanasayansi wamebaini kuwa kusugua meno kuna faida tele.

Wanasayansi wamegundua kuwa kutosafisha mdomo kunaweza kukusababishia maradhi ya ubongo, maarufu Alzheimer’s.

Huu ni ugonjwa wa ubongo ambao husababisha mwathiriwa kutofikiria, kusahau haraka na hata kushindwa kufanya kazi za kawaida.

Dalili za ugonjwa huu hujitokeza wazi mwathiriwa anapofikisha umri wa miaka 60.

Utafiti uliochapishwa katika jarida la watafiti wa masuala ya kisayansi, Science Advances, ulisema bakteria wanaosababisha ugonjwa wa fizi ndio husababisha maradhi haya.

Wanasayansi wanasema bakteria wanaosababisha ugonjwa wa fizi hutoa protini ambayo huathiri mishipa ya ubongo hivyo kumfanya mwathiriwa kuanza kuwa na shida ya kusahau.

Kulingana na watafiti hao, kuna uwezekano wa kuepuka maradhi haya iwapo watu watasugua meno na kusafisha mdomo mara kwa mara.

Wanasayansi walihusisha watu 53 waliokuwa na Alzheimer’s katika utafiti huo na wakabaini kwamba asilimia 96 walikuwa na bakteria wanaosababisha ugonjwa wa fizi.

Ugonjwa wa fizi umeorodheshwa nafasi ya 11 na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama mojawapo ya yanayoathiri idadi kubwa zaidi ya watu duniani.

Ugonjwa huo husababisha fizi kulegea hivyo watu kupoteza meno.

Kulingana na WHO, kula vyakula vyenye sukari nyingi pia husababisha maradhi ya fizi au mdomo.

Uvutaji wa sigara pia ni hatari kwa afya ya mdomo.