Kwa kuteua Karua, Raila alenga kura za wakazi wa Mlima Kenya, wanawake

Kwa kuteua Karua, Raila alenga kura za wakazi wa Mlima Kenya, wanawake

JUSTUS OCHIENG NA BENSON MATHEKA

HATUA ya mwaniaji urais wa muungao wa Azimio, Raila Odinga kumteua Bi Martha Karua kuwa mwaniaji wake imeibuka kuwa ishara ya jinsia na mabadiliko kuwa masuala makuu kwenye kampeni.

Uteuzi huo pia unaonyesha mkakati wa Bw Odinga wa kujitahidi kumega sehemu ya kura za eneo la Mlima Kenya, ambalo limekuwa likimkataa kwa wingi katika chaguzi nne za awali ambazo amewania mnamo 1997, 2007, 2013 na 2017.

Ikizingatiwa kuwa idadi ya wanawake ni karibu nusu ya waliosajiliwa kupiga kura, wanamikakati wa Azimio wana matumaini kuwa chaguo la Bi Karua litasaidia sehemu kubwa ya kura zao kote nchini bila kujali kabila.

Matarajio mengine ya Bw Odinga ni kuwa historia ya muda mrefu ya Bi Karua kama mtetezi wa utawala wa kisheria, demokrasia na haki utaonyesha kuwa Azimio ni muungano ulio na maono ya kuleta mabadiliko wanayohitaji Wakenya katika utawala na usimamizi wa taifa.

Hii inatarajiwa kutumiwa katika kampeni zao kama silaha ya kukabili mwaniaji urais wa Kenya Kwanza William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua kama wakereketwa wa utawala wa Kanu ambao ulinyanyasa wengi.

Wadadisi wa siasa pia wanaona chaguo la Bi Karua kuwa lenye lengo la kushawishi wapiga kura wa Mlima Kenya kumuunga mkono Bw Odinga.

“Karua ni chaguo la mwanasiasa thabiti ambaye atayumbisha kambi ya Ruto. Ana uwezo wa kushawishi wapiga kura wa eneo hilo kumpigia kura Raila,” akasema Prof Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multi Media jijini Nairobi.

Eneo la Mlima Kenya lina jumla ya kura 5,824,020 kutoka Meru (780,858), Tharaka Nithi (234,618), Embu (337,627), Nyeri (492,046), Kirinyaga (378,580) na Murang’a (628,416).Zingine zimo Kiambu (1,293,309), Laikipia (265,842), Nakuru (1,050,367) na Nyandarua (362,357).

Pia kuna wapiga kura wengi waliosajiliwa Nairobi ambao wanatoka eneo hilo.

Wakati huo huo, iwapo muungano wa Azimio la Umoja One Kenya utashinda uchaguzi mkuu ujao, idadi ya wanawake wanaoshikilia nyadhifa za juu serikalini itakuwa imeongezeka.

Wanaharakati wa usawa wa jinsia wanasema bali na kuwa wa pili kwa cheo baada ya rais, Bi Karua atakuwa mwanamke mwenye wadhifa wa juu serikalini.

“Huu utakuwa mwanzo wa kuafikia usawa wa jinsia na ushindi kwa wanawake ambao wamekuwa wakipigania washirikishwe katika nyadhifa za juu katika serikali,” asema mwanaharakati Sarah Apia.

Akimtangaza Bi Karua kuwa mgombea mwenza wake, Mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, pia alimtwika jukumu la waziri wa Haki na Maswala ya Katiba.

Hii itakuwa imeweka mfumo wa haki za nchini chini ya wanawake.

Jaji Mkuu Martha Koome ndiye mwanamke wa kwanza kuongoza idara ya Mahakama.

Naibu wake ni Jaji Philomena Mwilu ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Juu. Msajili Mkuu wa Mahakama ni Anne Amadi.

Wanawake wengine wanaoshikilia nyadhifa za juu serikalini ni Mhasibu Mkuu Nancy Gathungu, Msajili wa vyama vya kisiasa Ann Nderitu na Msimamizi wa Bajeti Margaret Nyakang’o.

Bi Apia anasema wanatarajia kuwa wanawake zaidi watashinda viti tofauti pamoja na kuteuliwa katika Baraza la Mawaziri, Mabalozi, Makatibu wa Wizara na Wakuu wa Mashirika ya Serikali.

“Tumeona wanawake wanaweza kuongoza mashirika ya serikali vyema. Rebecca Miano amesimamia KenGen hadi imepata ufanisi mkubwa,” akasema.Bi Miano amekuwa Mkurugenzi Mkuu wa KenGen kwa miaka minne sasa.

You can share this post!

Karua atambuliwa kwa misimamo thabiti kuhusu utawala wa...

Karua apaa Kalonzo akifunganya virago

T L