Michezo

Kwa Man Utd sherehe Liverpool ikirambwa

April 25th, 2024 2 min read

MANCHESTER, Uingereza

WACHEZAJI wa Manchester United wanafaa kukubali kukosolewa kama wanavyopongezwa tu, nahodha Bruno Fernandes amesema baada ya kusaidia mashetani wekundu kuponyoka na ushindi wa 4-2 dhidi ya Sheffield United, Jumatano.

Katika siku ambayo Liverpool walipata pigo katika vita vya kuwania taji kutokana na kichapo cha 2-0 kutoka kwa mahasimu wao Everton, Fernandes alisawazishia Manchester United 2-2 kupitia penalti dakika ya 61 kabla ya kuwaweka kifua mbele 3-2 kwa kusukuma kombora kali hadi wavuni dakika 20 baadaye.

Vijana wa kocha Erik ten Hag walikuwa wamejipata chini mara mbili dhidi ya Sheffield wanaovuta mkia kabla ya kuponyoka na ushindi huo.

Wachezaji wa Manchester United walikuwa wamekosolewa vikali baada ya kutupa uongozi wa mabao 3-0 katika nusu-fainali ya Kombe la FA mnamo Jumapili kabla ya kuzima Coventry City kwa njia ya penalti.

“Unaweza kuzoa ushindi mara tisa mfululizo, halafu upoteze mara moja pekee na utakosolewa vikali mno. Ukiwa United lazima ushinde kila mechi, hiyo ndiyo kazi yetu. Kama kuna mtu kikosini ambaye hajafahamu hilo, atalazimika kufanya hivyo. Lazima mchezaji yeyote wa Manchester United awe tayari kukosolewa na pia kupongezwa,” akaongeza.

Vijana wa Ten Hag, ambao hawakuwa wameshinda michuano minne mfululizo ya ligi, wamechupa hadi nambari sita baada ya kuchapa Sheffield. Watakabana koo na Burnley katika mechi ijayo hapo kesho.

Mahasimu wa jadi

Everton walizamisha vijana wa kocha Jurgen Klopp kupitia mabao ya Jarrad Branthwaite na Dominic Calvert-Lewin.

Ulikuwa ushindi wa kwanza ligini wa Everton dhidi ya Liverpool ugani Goodison Park tangu 2010.

Katika gozi hilo la Merseyside la 244, kipa Jordan Pickford alikuwa shujaa wa Everton baada ya kupangua shuti kadhaa hatari kutoka kwa Trent Alexander-Arnold, Darwin Nunez na Luis Diaz.

Kichapo hicho kilinyima Klopp fursa ya kuwa kocha wa kwanza katika historia ya Liverpool kupata ushindi mara 10 ligini dhidi ya Everton, ingawa kikubwa ni kuwa Liverpool inaonekana sasa kubanduliwa kwenye vita vya kutwaa taji la EPL.