Dimba

Kwa Manchester United, masaibu ni yale yale Liverpool wakiwacharaza 3 – 0

Na LABAAN SHABAAN August 4th, 2024 1 min read

MANCHESTER United ilitandikwa mabao matatu kwa nunge na Liverpool ambayo imekuwa na rekodi ya asilimia 100 katika ziara ya maandalizi Amerika.

Katika mechi iliyosakatwa mbele ya mashabiki 77,559 ugani Williams-Brice Stadium nchini Colombia, United itabaki kujilaumu sababu ya kuboronga mbele ya dimba.

Kutomakinika kwa kiungo mkabaji Casemiro kuliwapa vijana wa Arne Slot bao la kwanza dakika ya 10 kupitia Fabio Carvalho.

Dakika 20 baadaye Curtis Jones alikamilisha pasi ya Mohamed Salah ma kupanua mwanya wa uongozi.  

Katika kipindi cha pili kunako dakika ya 61, kipa wa United Andre Onana alishindwa kukaba shuti la Diogo Joto na kumtemea Konstantinos Tsimikas aliyefunga bao la tatu.

Mtihani wa United

Ulikuwa usiku wa giza totoro kwa Manchester United iliyolemewa na the Reds katika kukamilisha nafasi za kufunga.  

Difenda mchanga Will Fish alibebwa kwa machela alipoumia baada ya kumchezea vibaya Harvey Blair.

Ziara ya maandalizi kule Amerika imezalia Red Devils majeraha kwa wachezaji muhimu kama vile mshambuliaji Rasmus Hojland na mlinzi mpya Leny Yoro.

Wamepoteza mechi dhidi ya Arsenal na Liverpool – mahasimu wao wa ligi kuu ya kandanda Uingereza.

Hata hivyo United ilishinda dhidi ya Real Betis ya Uhispania kwa mabao 3 – 2.

United ilikuwa na nafasi bora za kushinda lakini Mason Mount na Amad Diallo walipoteza muda mbele ya kimia cha Liverpool na baadaye kupoteza nafasi za kutamba.

“Kuna sehemu tulifanya vizuri lakini sijafurahishwa na jinsi tunafungwa mabao,” alisema kocha Erik ten Hag.

Mwenzake wa Liverpool, Arne Slot, alisema mechi hiyo ingekamilika vingine: “Ni ushindi wa 3 – 0 lakini matokeo yangekuwa tofauti usiku huu.”