Makala

Kwa nini Mdjibouti ni tishio kwa Raila kuongoza AUC

Na CHARLES WASONGA September 1st, 2024 3 min read

INGAWA Rais wa Uganda Yoweri Museveni alidai kumwambia peupe Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Djibouti Mahmoud Youssouf kwamba atampigia kura Raila Odinga, waziri huyo anasawiriwa kama mpinzani wake mkuu katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Akihutubu katika hafla ya kumzindua Bw Odinga katika Ikulu ya Nairobi, Jumanne, Museveni, alifichua kuwa Youssouf alimtembelea kusaka kura yake lakini akamweleza peupe kwamba atamuunga mkono mwaniaji kutoka Kenya.

“Kabla ya kuanza safari ya kuja hapa kijana fulani kutoka Djibouti alinitembelea akaniambia ndiye mgombeaji wao wa kiti hiki na kwamba nimuunge mkono. Bila shaka, nilimsalimia kwa furaha, tukapigwa picha na tukanywa chai,” akasema.“Lakini nilimwambia napanga safari ya kuja Kenya kumuunga Raila kwa sababu ndiye mwaniaji bora zaidi kwa kazi hii,” Mzee Museveni akaeleza.

Rais huyo, ambaye amedumu mamlakani kwa miaka 38, alisisitiza kuwa wadhifa wa mwenyekiti wa AUC unahitaji mtu mwenye maono, moyo wa kujituma, uelewa mpana wa masuala yanayohusu Afrika na Waafrika.

Mbali na Youssouf na Bw Odinga, kiti hicho pia kimevutia aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Mauritius Anil Guyan na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Madagascar Richard Randriamandrato.

Wote wanapania kurithi kiti cha AUC baada ya Moussa Faki Mahamat kukamilisha kipindi chake cha kuhudumu Januari mwakani.

Wadadisi wachanganua

Lakini wadadisi wa masuala ya diplomasia na mahusiano ya kimataifa wanaonya kuwa Youssouf ndiye mpinzani mkuu wa Bw Odinga katika kinyang’anyiro kwa msingi wa kigezo cha miegemeo ya lugha.

Hii ni mbali na masuala mengine kama vile dini, umri, siasa za kimaslahi baina ya mataifa ya Afrika na maslahi ya kiuchumi nje ya bara hili katika mataifa ya Amerika, mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU), Urusi na nchi za bara Asia kama China, yanayotarajiwa kuathiri uamuzi wa marais wa Afrika watakaopiga kura Addis Ababa, Ethiopia.

Miongoni mwa nchi 54 za Afrika, lugha ya Kiingereza inazungumzwa kwa wingi katika nchi 24 nacho Kifaransa kinatumiwa katika nchi 28.

Aidha, lugha ya Kiarabu, ambayo pamoja na lugha hizo mbili, ni mojawapo ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika (AU), inazungumzwa kwa wingi katika karibu nchi 20.

Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha rasmi katika AU.

Kulingana na Mhadhiri katika Idara ya Diplomasia na Mafunzo ya Masuala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Nairobi Kizito Sabala mgombeaji atakayeungwa kwa idadi kubwa ya nchi zinazungumza lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu kwa wingi atakuwa na nafasi bora ya kuibuka mshindi.

“Ukweli ni kwamba miegemeo ya lugha imekuwa suala muhimu katika chaguzi zilizopita za AUC. Kwa hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba nchi ambako Kiingereza huzungumzwa kwa wingi zitamuunga mkono Bw Odinga na zile ambako Kifaransa kinazungumzwa sana zitaunga mkono ama Youssouf, Guyan wa Mauritius au Randriamandrato wa Madagascar,” anaeleza.“Isitoshe, mbali na Kifaransa kuzungumzwa Djibouti, Kiarabu kimekolea zaidi, hali ambayo itamfaidi pakubwa Bw Youssouf kwani huenda akapata uungwaji mkono kutoka nchi nyingi za Afrika Kaskazini, Afrika Magharibi na Afrika ya Kati ambako lugha hii imekita.”

Kauli yake inalandana na yake wakili James Mwamu anayeshauri kikosi cha kuendesha kampeni za Bw Odinga kuchukulia suala hilo, la miegemeo ya lugha miongoni mwa nchi za Afrika, kwa uzito mkubwa.

“Bara la Afrika limegawanywa vipande vitano, kimaeneo; Afrika Kaskazini, Afrika Magharibi, Afrika ya Kati, Afrika Kusini na Afrika Mashariki. Kwa kuwa mshindi katika uchaguzi huo anahitajika kupata uungwaji mkono kutoka nchi 34 kati ya 54 za Afrika, Bw Odinga anakabiliwa na kibarua kigumu kupata idadi hiyo ya kura na suala la lugha ni muhimu zaidi,” anaeleza.

“Kwa mtazamo huu, mwaniaji kutoka Djibouti anaweza kuwa tishio kwa Raila endapo atapata uungwaji mkubwa katika nchi za Afrika Kaskazini, Afrika Magharibi na Afrika ya Kati ambako lugha za Kifaransa na Kiarabu zinatumika zaidi,” anaongeza Bw Mwamu, ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Mawakili Afrika Mashariki (EALS).