Habari

Kwa nini mlinzi wa Ruto akafa?

February 22nd, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wameuliza maswali chungu nzima kuhusu kifo cha Sajini Kipyegon Kenei, aliyekuwa mmoja wa walinzi katika ofisi ya Naibu Rais William Ruto wakati washukiwa wa utapeli katika tenda feki ya silaha walipoitembelea.

Miongoni mwa maswali yasiyokuwa na majibu ni, kwa nini polisi walifikia uamuzi wa haraka kwamba afisa huyo alijiua bila kufanya uchunguzi na kwa nini wapelelezi hawakuandikisha taarifa kutoka kwa majirani wake katika mtaa wa Villa Franca, Nairobi?

Mwili wa Sajini Kenei ulipatikana kwenye nyumba yake Alhamisi alasiri ukiwa na jeraha la risasi. Kulingana na taarifa ya polisi, alijiua.

Hata hivyo, Wakenya hawakuridhirishwa na maelezo ya polisi hasa baada ya kubainika kuwa mlango wa nyumba ya afisa huyo ulikuwa wazi.

“Mtu anayepanga kujiua kwa kawaida huwa anajifungia ndani. Kwa kuwa mlango wa nyumba yake ulikuwa wazi, inazua maswali kuhusu kwa nini afisa huyo aliuawa,” alisema Mkenya mmoja kwenye Twitter.

Waliomfahamu afisa huyo walisema kwamba hakuwa mtu wa kufikiria kujiua.

“Nilifahamu kifo cha sajini Kenei kwa huzuni. Nilimfahamu kwa miaka mitano akiwa mlinzi wa Mheshimiwa Soita Shitanda na aliendelea kuwa rafiki baada ya kujiunga na walinzi wa Naibu Rais. Sifikirii alikuwa na akili za mhalifu,” alisema aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale.

Baadhi ya maswali ambayo Wakenya walitaka wapelelezi kuangazia katika uchunguzi wao ni kwa nini kifo chake kilitokea alipokuwa akitarajiwa kuandikisha taarifa kuhusu sakata hiyo katika ofisi ya Dkt Ruto huku wengine wakishuku huenda aliuawa mahali tofauti na mwili wake ukapelekwa kwake.

“Swali ni, kwa nini mlango wa nyumba yake ulikuwa wazi, nani aliuacha ukiwa wazi na ikiwa alijipiga risasi inavyodaiwa, mbona majirani hawakusikia mlio wa bastola?” aliuliza Mkenya mwingine.

Imeibuka kuwa polisi walifichua habari za kifo chake kabla ya kufahamisha familia yake inayoishi Nakuru.

Familia hiyo ilisema ilipata habari kupitia redio na ikapuuza madai kwamba alijiua.

Baba yake John Chesang alisema afisa huyo alitarajiwa kufanya harusi mwezi Agosti mwaka huu hivyo basi hakuamini macho yake aliposikia kuwa amejiua.

Kulingana na maelezo ya awali, Sajini Kenei alitakiwa kuandikisha taarifa kwa polisi kueleza jinsi aliyekuwa waziri wa michezo, Rashid Echesa na washukiwa wengine wanne walivyowaingiza raia wa kigeni katika ofisi ya Dkt Ruto, na hata kutia sahihi kandarasi feki ya kuuzia wizara ya ulinzi silaha.

Wakenya wanauliza ni habari gani alizokuwa nazo kuhusu sakata hiyo ambazo hakutaka zijulikane iwapo alijiua. Wengine wakawa wanajijazia kuwa kiwa alimalizwa, basi waliomuua hawakutaka zijulikane iwapo angeandikisha taarifa.

Habari za kifo chake zilijiri siku moja baada ya Dkt Ruto kumtaka Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai kuchunguza walinzi waliokuwa kazini wakati Echesa na washukiwa wenzake walipoingia katika jumba la Harambee Annexe.

Dkt Ruto alimwomboleza Sajini Kenei akimtaja kama afisa wa polisi aliyekuwa na nidhamu ya juu kazini.

“Kenei alikuwa afisa wa polisi mwenye umri mdogo na mwenye nidhamu. Ninaomba idara zinazohusika kuchunguza alivyokufa,” alisema Dkt Ruto.

Mbali na kutilia shaka maelezo ya polisi, Wakenya mtandaoni hawakuridhishwa na hatua ambazo ofisi ya Dkt Ruto ilichukua pale Sajini Kenei alipokosa kufika kazini Jumatano na kujiwasilisha kwa wapelelezi kuandikisha taarifa.

Wanasema ikizingatiwa kuwa kulikuwa na uchunguzi muhimu uliokuwa ukiendelea, hatua ya kwanza ingekuwa ni kufika kwake mapema kubaini hali yake.

Kabla ya mwili wa afisa huyo kupatikana Alhamisi alasiri, ofisi ya Ruto ilikuwa imetoa taarifa ikisema kwamba alikuwa ametoweka.

Mara yake ya mwisho kuonekana akiingia katika mtaa au nyumba yake ilikuwa lini? Kuna walinzi katika malango ya mtaa wa Villa Franca?

Je, walimuona mgeni yeyote baada yake kuingia au siku hiyo?

Je, mtu wa mwisho kuwasiliana na Kipyegon ni nani? Ni baadhi ya maswali ambayo Wakenya waliuliza kwenye mitandao ya kijamii.

Walitilia shaka taarifa ya polisi kwamba mwili wake uligunduliwa kufuatia harufu mbaya kutoka nyumba yake wakisema haiwezi kuaminika.