Michezo

Kwa sasa ni mlima kwa Arsenal kutinga nne bora EPL – Unai Emery

January 14th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Arsenal Unai Emery amekiri kwamba ndoto ya klabu hiyo kutinga timu nne bora mwishoni mwa msimu huenda isitimie baada ya kichapo cha 1-0 Jumamosi Januari 12 dhidi ya majirani wao West Ham.

Bao safi la Declan Rice ambalo lilikuwa lake la kwanza katika ligi kuu nchini Uingereza(EPL) lilizamisha zaidi chombo cha Arsenal ambao sasa wamepata alama moja tu katika mechi zao nne mtawalia.

Ushindi wa majirani wao Chelsea dhidi ya Newcastle United ugani Stamford Bridge ulipelekea mwanya wa alama sita kutamalaki kati yao na Arsenal huku mbio za kuwania kumaliza ndani ya mduara wa nne bora na kufuzu kushiriki klabu bingwa msimu ujao wa 2019/20 zikiendelea kushika kasi.

Mahasimu wao Manchester United nao wapo alama sawa na Arsenal baada ya kutwaa ushindi muhimu wa 1-0 dhidi ya Tottenham Hot Spurs ugani Wembley Jumapili.

“Kwa sasa mambo yanazidi kutuwia magumu. Hata hivyo kilicho muhimu ni tusipoteze dira  na tujiamini kwa zaidi ya michuano 38 tuliyosalia nayo katika mashindano mbalimbali,” akatanguliza Unai

“Ni matokeo mabaya. Tunacheza dhidi ya Chelsea Jumamosi 19 na lazima tushinde ili turejeshe matumaini na kufidia alama tulizopoteza kwenye mechi za awali,” akaongeza mkufunzi huyo baada ya mechi ya West Ham.

Fomu ya Arsenal katika mechi za ugenini imekuwa mbovu sana na ndiyo Imechangia wao kufikiwa na Manchester United kwenye  msimamo wa jedwali la ligi.

Iwapo Arsenal watakosa kutinga nne bora, basi watakosa kushiriki mechi za klabu bingwa barani Uropa kwa mwaka wa tatu mfululizo.