Habari

Kwaheri Prof Walibora

April 22nd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

ULIMWENGU ni jukwaa la pekee kwetu sote kuigizia tamthilia inayoitwa ‘Maisha’ – mchezo ambao siku zote mwelekezi wake ni Mwenyezi Mungu aliye chanzo cha uhai na vipaji vyote tulivyonavyo.

Mchezo huu unajumuisha maonyesho matatu ambayo ni mwanadamu kuzaliwa, kuoa au kuolewa kisha kuaga dunia.

Kipindi cha zaidi ya wiki moja na nusu kimepita tangu jamii nzima ya wapenzi, wakereketwa na watetezi wa Kiswahili ipate pigo kubwa kutokana na kifo cha msomi, mwalimu, mwanahabari na mwandishi maarufu Profesa Kennedy Waliaula Athanasias Wafula Walibora.

Sauti iliyopasua mawimbi kila alipojipata nyuma ya bomba; mbinu ya kalamu iliyokosoa na kuielekeza jamii ipasavyo pamoja na umilisi mpana wa Kiswahili ni upekee uliomtambulisha Prof Walibora na kumkweza ngazi kitaaluma.

Ungemsikia siku zote akicheza na maneno, akitumia misemo, nahau, methali na tamathali nyinginezo za lugha akitangaza mpira redioni na akisoma taarifa za habari runingani.

Ubunifu wake ulikuwa wa kiwango cha juu na uwezo wa kutumia lugha kwa ufundi mkubwa ni sifa iliyodhihirika wazi katika makala aliyoyaandika magazetini na matopa kwa matopa ya vitabu alivyovitunga.

Kuzikwa kwa Prof Walibora hii leo ni mwanzo wa kusadiki ukweli mchungu unaoghasi, kuchosha na kuvunja moyo – kwamba kifo kimetupokonya johari adhimu na kito adimu chenye thamani kubwa isiyo na mfano katika ulingo wa akademia, tasnia ya uanahabari na bahari ya uandishi wa kazi za kibunifu.

Hata baada ya kuzikwa nyumbani kwao katika kijiji cha Bonde Makutano Kwa Ngozi, eneo la Cherangany, Kaunti ya Trans-Nzoia; mchango wa Prof Walibora hauwezi kusahaulika kamwe katika majukwaa ya makuzi ya Kiswahili.

Katika vingi vya vitabu vyake, Prof Walibora alipania kumkweza mnyonge na kumpa sauti licha ya panda-shuka za kila sampuli maishani kutishia kabisa kumzimia mshumaa wa matumaini yaliyoning’inizwa kwenye uzi mwembamba wa imani katika ulimwengu huu.Guru Ustadh Wallah Bin Wallah anasema hivi:

“Saa moja kuishi, saa moja kuisha. Laiti mwanadamu angalijaliwa uwezo wa kujua na kuyaelewa mambo mazuri au mabaya yatakayokuja au yatakayomfika katika siku zijazo kuanzia wakati huu anapovuta pumzi!

Hakika angalijiandaa zaidi kuyakabili yajayo ama angaliyasema na kuyatenda yote anayopaswa kutenda wakati angali hai duniani!Ndugu Prof Ken Walibora ametuacha baada ya kufanya kazi adhimu alizofanya katika juhudi za kukikuza na kukiimarisha Kiswahili.

Lakini ukweli ni kwamba bado alikuwa na majukumu na uwezo mwingi sana wa kutoa mchango katika mawanda ya Kiswahili bila kinyongo kutokana na bidii zake, uadilifu wake, busara zake, ufasaha wake, wema wake, tajriba yake pamoja na upendo wake katika lugha ya Kiswahili.

Kwaheri Ndugu Ken Profesa Walibora! Umetuachia ukiwa na biwi la simanzi sisi wafiwa wa Kiswahili!Labda njia moja ya kumpa tunu Prof Walibora si kuomboleza kifo chake, bali ni kutafakari kuhusu upekee wa mchango wake katika uwanja wa fasihi ambao aliuchangamkia kwa dhati.

Prof Walibora ameaga dunia wakati ambapo taaluma ya Kiswahili bado inamhitaji mno. Alipenda Uafrika na alivumisha falsafa hiyo katika tungo zake.

Jina la Prof Walibora halitawahi kukosekana katika orodha ya watetezi na wafia-lugha waliojihini, kujihimu na kujikusuru kwa hali na mali kuchangia ustawi na maendeleo ya Kiswahili.

Kuondoka kwake ni msiba mkubwa mioyoni mwa wapenzi wa Kiswahili na pengo aliloliacha kitaaluma haliwezi kuzibika.

Alikuwa mpole, mzungumzaji mwenye staha, mwandishi aliyejiamini na msomi aliyetawaliwa na shauku ya kung’ang’ania elimu.

Tunapovuta taswira ya safari ya maendeleo ya Kiswahili kwa kipindi cha zaidi ya miongo miwili iliyopita, hapana shaka kwamba mchango wa Prof Walibora unaonekana kuacha taathira kubwa mno katika tanzu zote za Fasishi Andishi – riwaya, tamthilia, hadithi fupi, hadithi za watoto, ushairi na tawasifu.