Habari

Kwaheri wangwana

August 4th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

GAVANA wa Bomet, Dkt Joyce Laboso, Jumamosi alizikwa kishujaa katika boma lake lililoko Fort Ternan, Koru, Kaunti ya Kisumu huku akitajwa kama kiongozi muungwana na mwadilifu ambaye alijitolea kuwahudumia wananchi.

Dkt Laboso aliandaliwa mazishi ya kitaifa yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali serikalini, wakiwemo Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, magavana, maseneta, wabunge kati ya viongozi wengine.

Sawa na ilivyokuwa katika ibada zilizotangulia Nairobi na Bomet, maelfu ya wananchi pia walijitokeza kwa wingi kumuaga gavana huyo aliyeaga dunia kutokana na maradhi ya kansa.

Rais Kenyatta alizua msisimko kwa muda, alipowasili kwa ndege mbili za kijeshi.

Wazungumzaji mbalimbali walisisitiza haja ya viongozi na Wakenya kudumisha umoja na uadilifu, vilivyotajwa kuwa vigezo vikuu alivyodhihirisha Dkt Laboso katika uhai wake.

Rais Kenyatta alimtaja kama mfano bora wa uadilifu na uwajibikaji kwa viongozi wengine, ikizingatiwa kuwa hakuwaajiri jamaa zake wala kuwahusisha katika masuala ya usimamizi wa Kaunti ya Bomet.

“Joyce alikuwa mfano wa kuigwa kwani hakutoa kandarasi kwa jamaa zake, licha ya kuwa na uwezo na nafasi ya kufanya hivyo. Hilo linatuonyesha kiwango cha uadilifu aliokuwa nao,” alisema Rais Kenyatta.

Vilevile, aliwatahadharisha Wakenya dhidi ya viongozi, aliosema huwa vitendo vyao haviambatani na kauli zao.

“Hebu tuwe watu wanaomaanisha na kutenda tunayoyasema. Tusiwe wale ambao Yesu alisema wanahubiri maji na kujiingiza katika vitendo vya giza jioni. Shauri yenu, mtajionea mengi,” alitahadharisha.

Dkt Ruto alimtaja marehemu Laboso kama kiongozi wa kipekee, ikizingatiwa kwamba aliweka rekodi kwa kila nafasi aliyochaguliwa.

“Dada yetu Laboso alikuwa mtu jasiri, ambaye alionyesha ukakamavu mkubwa kwa kila nafasi aliyohudumu, bila kujali alikuwa akiugua saratani. Kuchaguliwa kwake kama mbunge wa Sotik, Naibu Spika wa kwanza mwanamke katika Bunge la Kitaifa na hatimaye kuwa miongoni mwa magavana wa kwanza wanawake kunaonyesha mfano wa kiongozi aliyeonyesha ushujaa wa kipekee,” alisema Dkt Ruto.

Raila aunga mkono

Kwa upande wake, Bw Odinga aliwaunga mkono magavana Anne Waiguru (Kirinyaga) na Charity Ngilu (Kitui) katika wito wao wa kumtaka Naibu Gavana wa Bomet Dkt Hillary Barchok kumteua mwanamke kuwa naibu wake.

Magavana hao walisema kuwa hiyo ndiyo njia pekee ambayo kaunti hiyo itaonyesha heshima kwa marehemu.

Bw Odinga aliomba kupitishwa kwa Sheria ya Kuwatetea Wanawake, ili kuhakikisha kuwa hawatumii muda wao mwingi kurai jamii kuwapa nafasi za uongozi.

Gavana wa Kisumu Anyang Nyong’o aliiomba serikali kuweka mikakati ya kutoa mafunzo kwa wataalamu zaidi wa saratani, akitaja hilo kama njia ya pekee ambapo Kenya itaweza kuukabili ugonjwa huo.

Mumewe Dkt Edwin Abonyo, wanawe, jamaa na marafiki walimsifu marehemu kwa moyo wa kujali na bidii yake.

Wanawake waliimba na kucheza wakizunguka jeneza lililobeba mwili wake huku Rais Kenyatta akijumuika nao.

Dkt Laboso alifariki Jumatatu katika Hospitali ya Nairobi, alikokuwa akipokea matibabu ya saratani.

Alikuwa ametibiwa nchini Uingereza na India kabla ya kurejeshwa nchini.