Habari Mseto

Kwale kusimamia bandari ya Shimoni

September 14th, 2019 2 min read

Na FADHILI FREDRICK

KAUNTI ya Kwale imekuwa ya kwanza kunufaika na ahadi za Rais Uhuru Kenyatta kwa viongozi wa Pwani, baada ya Halmashauri ya Bandari nchini (KPA), kusema itakabidhi usimamizi wa bandari ya Shimoni kwa serikali ya kaunti.

Bandari hiyo inajengwa kwa gharama ya Sh20 bilioni.

Hatua hiyo ilibainika katika mkutano wa mashauriano uliyofanyika Alhamisi Kwale ukioongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Dkt Daniel Manduku na kuhudhuriwa na Gavana Salim Mvurya na Naibu wake Fatuma Achani.

“Tutatoa karibu operesheni zote za bandari kwa usimamizi wa Serikali ya Kaunti ya Kwale. Tutabaki na sehemu ya kiufundi. Tutaweka makubaliano na Kaunti ya Kwale,” akasema Bw Manduku.

Bw Manduku alisema waliiga mfumo wa kukabidhi usimamizi wa rasilimali kwa serikali za majimbo kutoka Ushelisheli baada ya kufanya ziara nchini humo.

Hatua hiyo pia inajiri siku chache baada ya Rais Kenyatta kuzuru bandari ya Shimoni kwenye mpaka wa bahari ya Kenya na Tanzania ambayo itajengwa kupitia ushirikiano wa umma na sekta ya kibinafsi (PPP).

Gavana Mvurya aliunga mkono hatua ya KPA kukabidhi usimamizi wa bandari kwa kaunti akisema utawala wake utashirikiana na halmashauri hiyo.

“Nataka kuhakikishia ushirikiano wa serikali yangu kwa jumla kwa hatua zote za ujenzi wa bandari hiyo ambayo itabadilisha uchumi wa eneo hili,” akasema Bw Mvurya.

“Tunataka mpango kamili wa kujenga uwezo ambao utawezesha Kaunti kutekeleza usimamizi wa bandari vizuri,” akasema Bw Manduku.

Tunajua pia kuwa bandari itatoa fursa nyingi kwa watu. Tunawataka pia wafahamu jinsi wanaweza kutumia fursa hizi,” akasema.

Bw Manduku alisema KPA itawezesha mpango huo kikamilifu na usimamizi kuandaa orodha kamili ya maeneo ambayo ni muhimu kutekeleza zoezi hilo.

Ushirikiano

Bi Achani alisema KPA inahitaji kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Kaunti ya Kwale ili kufuatilia haraka zoezi hilo ambalo tayari linatekelezwa na serikali ya kitaifa.

“Hatutaki hali ambayo migogoro itaibuka kati ya KPA na wananchi kama ilivyotokea wakati wa zoezi la uzoaji mchanga kutoka ufuo wa Diani,” akasema.

Gavana Mvurya alisisitiza kwamba lazima kamati iundwe ili kuongoza mchakato wa kusimamia mradi huo.

“Hii inapaswa kutumika hata kwa mradi wa Dongo-Kundu. Watu wa Kwale wanapaswa kuhusika kikamilifu na kuambiwa watakavyofaidika na miradi mikubwa kama hiyo,” akasema Gavana.

Bw Manduku alimhakikishia Gavana kuwa mchakato wa utekelezaji wa miradi hiyo utakuwa wa mashauriano. Pia alisema kamati ya maafisa 10, watano kutoka kila upande, itaundwa.

Vile vile, alisema afisi ya kamishna wa kaunti itahusika kuiwakilisha serikali ya kitaifa.