Habari Mseto

Kwale yaibuka bora zaidi katika mpango wa ajira kwa vijana

May 30th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

KAUNTI ya Kwale imetajwa kuwa bora zaidi katika kuimarisha mpango wa serikali kuu wa kuwapa ajira vijana maarufu ‘Kazi Mtaani’.

Gavana wa Kwale Salim Mvurya Salim Mvurya alipongezwa kwa juhudi zake za kuhakikisha mpango huo unawanufaisha vijana katika kaunti yake.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu katika Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Mijini Bw Charles Hinga, Kaunti ya Kwale ndiyo bora zaidi katika uimarishaji wa mpango huo wa serikali.

Katika kipindi cha wiki tatu zilizopita takriban vijana 1,000 wamenufaika katika mpango wa ‘Kazi Mtaani’ unaonuia kusaidia vijana kujikimu kimaisha kufuatia janga la virusi vya corona ambalo limelemaza ajira na uchumi wa nchi.

“Mpango  huu ulianzishwa kaunti sita Kwale ikiwa mojawapo lakini imefanya vyema zaidi huku Gavana Mvurya akionyesha uongozi bora baada ya kukumbatia mpango huu ili kuhakikisha vijana wananufaika. Matunda yake yanaonekana; Kwale imekuwa safi zaidi,” alisema Bw Hinga.

Pia aliwahakikishia vijana kwamba wataendelea kunufaika na mpango huo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kwamba awamu ya pili ambayo itaajiri zaidi ya vijana laki 200,000 kaunti kadhaa.

Kwa upande wake, Bw Mvurya alimshukuru Rais Kenyatta kwa kubuni mpango huo ambao unaendelea kuhakikisha vijana wananufaika kwa mapato ya kujikimu.

“Tunafurahi kutajwa bora zaidi kwenye awamu ya kwanza, tunaunga mkono na kushirikiana na serikali kuu licha ya janga hili la corona tunafurahi kwamba wakazi wetu wanapata ajira ,” alisema Bw Mvurya.

Bw Hinga ni miongoni mwa viongozi wa serikali kuu waliozuru Kwale kutathmini mpango huo.

Kwenye awamu ya kwanza vijana walijishughulisha na usafi wa mazingira na kuzibua mitaro ya majitaka.