Makala

Kwangu ni kazi tu, asema mpasuaji mkuu wa maiti

February 16th, 2024 2 min read

NA LEON LIDIGU

KWA miaka mingi Daktari Mkuu wa serikali anayehusika na upasuaji wa maiti, Dkt Johansen Oduor, amekuwa akifanya upasuaji wa miili nchini, wengi wakimheshimu kutokana na huduma ambazo amekuwa akitoa wakati wa mauti.

Dkt Oduor kwenye mahojiano na Taifa Leo, alifichua kuwa amepasua maelfu ya maiti kwa muda wa miaka 16 ambayo amekuwa akifanya kazi hiyo na ana ienzi sana jinsi tu watu wengine wanavyothamini ajira zao.

Anasema msukumo ambao amekuwa akipata ni kuhakikisha kuwa familia za marehemu zinafahamu kilichosababisha mauti ya wapendwa wao badala ya suala hilo kusalia kama kitendawili.

“Napenda watu ambao wameaga dunia kwa sababu ikilinganishwa na binadamu wengine, miili huwa haiumizi mtu. Utaupata mwili mahali ambapo uliuacha,” akasema Dkt Oduor.

Mwanapatholojia huyo amepasua miili 429 iliyofukuliwa Shakahola lakini kilichomshangaza na kumwacha na makovu zaidi rohoni, ni jinsi msichana Rita Waeni alivyouawa katika chumba cha kukodisha kwa muda mtaani Roysambu.

“Kwa muda ambao nimefanya kazi hii, sijaona uchungu na mauaji ya kikatili kama yale. Waliomuua Waeni walijaribu kufuta kila aina ya ushahidi kwa kumng’oa kucha,” akaongeza.

Dkt Oduor alikulia mtaa wa Eastlands na kusomea Shule ya Upili ya St Aquinas kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi ambako alisomea matibabu na upasuaji.

Baadaye alienda kwa masomo zaidi Afrika Kusini kabla ya kurejea nyumbani na kujiunga na Wizara ya Afya.

“Bosi wangu wakati huo aliona kipaji changu na akanifanya naibu wake kisha nikachukua usukani alipoondoka,” akasema.

Mtaalamu huyo wa masuala ya upasuaji wa maiti hata hivyo, alikataa kuzungumzia familia yake akisema huwa hazungumzii maisha yake na watu wake.

Alifichua kuwa alianza kuwa na msukumo wa kupasua miili akikua Eastlands kutokana na mauaji yaliyokuwa yakishuhudiwa mara kwa mara mtaani humo.

“Nilikuwa nasikia na kuwaona watu wakililia haki ambayo hawakuipata. Niliamua kuchukua mkondo wa kutumia sayansi ili wapate haki hiyo,” akasema.

Pia akiwa mdogo, alipenda sana kuona sinema za uchunguzi wa visa vya uhalifu na akapenda jinsi ambavyo makachero kwenye baadhi ya video hizo walikuwa wakipata suluhu kwa mauaji na uhalifu.

“Nilipenda sana kutazama sinema ya CSI nikikua na uchunguzi uliokuwa ukiendelea kwenye sinema hiyo ulinivutia sana,” akasema.

Hii leo, daktari huyo wa upasuaji wa maiti anaishi maisha ambapo anakiri ametimiza ndoto yake ya utotoni na anasema upasuaji huo haujamwathiri kivyovyote kiakili.

“Wakati ambapo nilikuwa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Nairobi, nilikuwa naishi kwenye maabara kwa muda wa miaka miwili. Uoga huo ulipotea kabisa na sasa nafanya kazi hii kama tu kazi nyingine,” akasema.