Michezo

Kwemoi afungiwa na corona

July 21st, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

RODGERS Kwemoi amekiri kwamba janga la corona lilimbishia na fungu la matatizo ambayo kwa sasa yanatishia kabisa kulemaza taaluma yake.

Mbali na kukosa fursa ya kushiriki marathon yake ya kwanza kitaaluma, mshindi huyo wa nishani ya shaba katika mbio za mita 10,000 kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola, pia amekwama nchini na hawezi sasa kurejea kazini pake Japan.

Kwemoi amekuwa akikimbilia kikosi cha Aisan Kyobio cha Japan kilichomsajili mnamo 2015. Ujio wa virusi vya corona sasa umetatiza safari yake ya kurejea Japan kutokana na masharti yanayodhibiti safari za ndege kutoka na kuingia humu nchini.

“Nilitarajia kurejea Japan mnamo Machi 25, 2020. Ilisadifu kwamba hiyo ndiyo siku ambapo safari zote za kimataifa zilipigwa marufuku,” akasema Kwemoi ambaye kwa sasa hujifanyia mazoezi katika eneo Furfural, Kaunti ya Uasin Gishu.

Kwemoi ambaye pia ni bingwa wa zamani wa dunia katika mbio za mita 10,000, sasa anapania kuzoa medali ya dhahabu katika kivumbi hicho kwenye Olimpiki zijazo za Tokyo nchini Japan.

Naftali Temu ndiye Mkenya wa mwisho kuwahi kutwaa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki za 1968 nchini Mexico. Charles Kamathi ndiye Mkenya wa mwisho kutamalaki mbio hizo kwenye Riadha za Dunia zilizofanyika jijini Edmonton, Canada. Hiyo ilikuwa dhahabu ya tatu kwa Kenya tangu Paul Koech (1983) na Moses Tanui (1991).

“Ninaazimia kushiriki mbio kadhaa za marathon, zile za mita 5,000 na mita 10,000. Hata hivyo, kubwa zaidi katika matamanio yangu ni kuzoa dhahabu katika mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki zijazo,” akasema Kwemoi.

Nafuu kubwa zaidi kwa Kwemoi ni kwamba yeye ni miongoni mwa wanariadha sita wa Kenya walionufaika kifedha kutoka kwa Kamati ya Olimpiki ya bara la Afrika (ANOCA). Anasema ufadhili huo utamsaidia pakubwa kujiandaa kwa Olimpiki za Tokyo, Japan.

Mbali na Kwemoi, wengine walionufaika na ufadhili huo ni bingwa wa Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 800 Wycliffe Kinyamal, Emily Cherotich Tuwei wa mbio za mita 800 na mshindi wa medali ya shaba katika mbio za mita 800 kwenye Riadha za Dunia, Ferguson Rotich.

Wengine ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Conseslus Kipruto na bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot.

Wanariadha hao wamekuwa wakipokea Sh400,000 kila mmoja kwa mwezi tangu mwisho wa Juni 2020. Ufadhili huo utakatika Juni 23, 2021 takriban siku 30 kabla ya Olimpiki za 2021 kuanza.

Kwemoi aliingia katika sajili rasmi ya Aisan Kyobio kwa usaidizi wa bingwa wa zamani wa mbio za nyika barani Afrika, Leonard Barsoton aliyeridhishwa na jinsi alivyotifua kivumbi kwenye makala ya 41 ya Mbio za Nyika za Dunia nchini China mnamo Machi 2015.