NA AREGE RUTH
MABINGWA mara tatu Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) Vihiga Queens, wamepoteza mechi yao ya pili msimu huu waliponyoroshwa 3-2 na Ulinzi Starlets katika uwanja wa Mumias Sports Complex leo Jumamosi.
Kwenye mechi ya awali ya ligi, Vihiga walipoteza (4-1) dhidi ya mabingwa watetezi Thika Queens nao Ulinzi wakapigwa (1-0) na WADADIA Women ugani Ulinzi Sports Complex.
Mshambuliaji wa Vihiga Ikalakala Sharlyne alicheka na wavu mara mbili dakika ya 20 na 60.
Nao washambuliaji Lucy Nato, Joy KingLady na Sophia Adhiambo wakafungia Ulinzi dakika za 30, 42 na 90 mtawalia.
Vihiga wamepata pigo kubwa kwenye mechi hiyo baada ya kipa wa kwanza Dianah Tembesi kupata jeraha na nafasi yake ikachukuliwa na kipa Sophie Akinyi katika kipindi cha pili.
Ushindi huo umeipeleka Ulinzi hadi nafasi ya nne na alama 13 kutokana na mechi nane. Vihiga inaendelea kusalia kileleni mwa jedwali ikiwa na alama 16 baada ya mechi nane.
Kocha wa Ulinzi Joseph Mwanzia amesema,”Ilikuwa ni mechi ngumu sana kwetu. Nashukuru wachezaji wangu kwa kuonyesha mchezo mzuri. Huu ni ushindi muhimu kwetu ikizingatiwa kwamba tulikuwa tumepoteza mechi mbili za awali.”
Ugani Kenyatta mjini Kitale, wenyeji Trans Nzoia Falcons walitoshana nguvu ya 0-0 na Zetech Sparks.
Baada ya sare hiyo, timu hizo zimeshikilia nafasi ya nane na tisa kwenye jedwali zikiwa na alama nane na tisa mtawalia.
Kwa upande wa Falcons ambao wana mechi moja kibindoni, kocha wa timu hiyo Justine Okiring anasema, bado ana kazi ngumu ya kujenga timu upya.
“Tulipata nafasi za wazi tatu lakini hatukufanyia kazi. Kijumla, sote tulitoshana nguvu na wapinzani wetu. Bado tuna kazi ya kufanya kwenye timu yetu kwa sababu wachezaji wengi bado hawajarejea kujiunga na timu,” amesema Okiring.