Michezo

KWPL: Wadadia LG kusaka ushindi wikendi

June 6th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

WADADIA LG wikendi hii itakuwa vitani kutafuta pointi sita muhimu itakaposhiriki mechi mbili kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake ya Kenya (KWPL) msimu huu.

Wadadia LG ambayo hutiwa makali na kocha, Richard Sumba inayokamata nafasi ya nane Jumamosi itakuwa ugenini mjini Kisumu kucheza na Kisumu All Stars ya nne kwenye jedwali. Kisha Jumapili itazuru mjini Kakamega kumenyana na Nyuki Starlets katika uwanja wa Approved School.

”Nimeandaa wasichana wangu tayari kukabili wapinzani wetu kwenye juhudi za kutafuta alama sita muhimu ili kujiongezea matumaini ya kumaliza nafasi bora msimu huu,” kocha wa Mumias alisema na kuongeza kwamba kampeni za msimu huu zinazidi kushuhudia ushindani mkali.

Katika ratiba hiyo mchezo mgumu unatazamiwa kushuhudiwa Jumapili pale malkia wa soka nchini, Vihiga Queens itakapoalika Trans Nzoia Falcons uwanjani Mumias Sports Compex mjini humo.

Trans Nzoia Falcons itateremka dimbani ikijivunia kuibandua GASPO Women kileleni ilipoizima mabao 2-0 wiki iliyopita.

Kwenye mfululizo wa mechi hizo, Thika Queens itakuwa ugenini mjini Nairobi kuvaana na Kayole Starlets uwanjani Camp Toyoyo Jericho.

Nayo Makolanders itakwaruzana na Eldoret Falcons, Kibera Girls Soccer Academy (KGSA) itazuru mjini Ruiru kucheza na Soccer Queens huku Spedag FC ikionana uso kwa macho na Mathare United Women uwanjani Camp Toyoyo Jericho, Nairobi.