Habari Mseto

KWS yamwokoa mwanapundamilia akinyonya maziwa ya mzoga wa mamake

January 24th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

WAKENYA wameguswa kuona mtoto wa pundamilia akinyonya maziwa ya mama yake aliyefariki jangwani eneo la Lengardae, Kaunti ya Samburu.

Mnamo Jumatatu Januari 22, 2024, madaktari wa wanyama wanaotembea walimwokoa pundamilia kinda katika tukio la kugusa moyo.

Hata maafisa hao wa Shirika la Wanyamapori (KWS) walipokuwa wanamwokoa, pundamilia huyo alikuwa anaendelea kunyonya titi kavu la mzoga wa mama yake aliyekuwa tayari amekata roho.

Pundamilia huyo alikufa baada ya kujifungua mtoto huyo ambaye alikutwa anahangaikia maisha katika siku zake za kwanza duniani.

Matabibu tamba wa KWS walimpeleka punda kinda huyo katika Hifadhi ya Wanyama ya Reteti.

Uokozi huu uliofanikiwa haukusaidia tu punda huyo bali pia ulisisitiza kuhusu umuhimu wa kulinda viumbe wa porini,” ilisema taarifa ya KWS kwenye akaunti yao ya mtandao wa kijamii wa X (awali Twitter).

Watumiaji wa mitandao ya kijamii waliguswa sana na tukio hili.

“Hii ni hali ya kuhuzunisha sana na hatua ya KWS kumuokoa imenigusa moyo sana,” alieleza Joseph Mus.

Mwingine kwa jina Kassim Macella alisikitika: “Wanyama wa mwituni wanateseka sana kwa magonjwa na matatizo mengine. Wizara ya Huduma ya Pori inajua kufyonza pesa tu. Licha ya kumegewa fedha nyingi, wanyama hunywa maji tu katika misimu ya mvua.”