Michezo

Kyle Walker atarajia mtoto na mwingine baada ya kutemwa

February 13th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WIKI moja baada ya Kyle Walker kutemwa na mke wake Annie Kilner kwa kuchuna ngozi mwigizaji wa vipindi runinga Laura Brown, beki huyo wa Manchester City anasemekana anatarajia mtoto na mwanamitindo Lauryn Goodman.

Mwanzoni, gazeti la Sun lilidai kuwa Goodman alikuwa amepachikwa mimba na mchezaji mmoja kutoka Ligi Kuu ya Uingereza bila kutaja jina lake, lakini sasa mwanamitindo huyo amemwaga mtama.

“Nataka kuweka mambo sawa kwa sababu napokea jumbe nyingi ambazo zinanisukuma niseme baba ya mtoto ninayetarajia.

“Nimesumbuliwa sana na hali hii imeniletea msongo wa mawazo nikisalia na miezi mitatu nijifungue. Fununu zimeanza kuenea na ningependa watu wapate kusikia kutoka kwangu ili wakome kupayuka.

“Kyle Walker na mimi tunatarajia mtoto mwezi Aprili na tulifanya tendo la ndoa tukiwa tumetengana na wapenzi wetu wa zamani.

“Hii itakuwa mara ya mwisho nazungumzia suala hili na kutoka sasa, nitazungumza mambo mengine ya maana.”

Lauryn aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wakala na kakake mshambuliaji wa Manchester United Marcus Rashford, Dane.

Hata hivyo, uhusiano wa Lauryn na Dane haukudumu, huku Walker akiaminika kuanzisha uhusiano na Lauryn karibu mwaka mmoja uliopita na sasa wanatarajia mtoto wa ‘kimiujiza’.

Iliripotiwa awali kuwa Lauryn, 29, aliambiwa na madaktari kuwa hawezi kupata mtoto kwa njia ya kawaida.

Walker,28, alipata watoto wawili na Kilner,26, ambaye alikuwa mpenzi wake kwa miaka 10. Laura, 30, alianika Walker kwa Kilner baada ya kugundua alikuwa katika uhusiano na Kilner ambao hakuwa amemueleza.