Michezo

Kylian Mbappe kusalia mkekani kwa wiki tatu kuuguza jeraha

July 28th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI chipukizi wa Paris Saint-Germain (PSG), Kylian Mbappe atakosa robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) itakayowakutanisha na Atalanta ya Italia jijini Lisbon, Ureno mnamo Agosti 12, 2020.

Mbappe, 21, alipata jeraha baya la kifundo cha mguu wa kulia wakati wa fainali ya kuwania taji la French Cup iliyowakutanisha PSG na Saint-Etienne mnamo Julai 24, 2020 uwanjani Stade France.

Nyota huyo mzawa wa Ufaransa sasa atasalia mkekani kwa jumla ya majuma matatu.

PSG waliibuka washindi wa mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki 5,000. Walifunga bao la pekee na la ushindi kupitia kwa fowadi mahiri mzawa wa Brazil, Neymar Jr.

Mbappe anatarajiwa kurejea kutambisha PSG katika soka ya UEFA mnamo Agosti 18, 2020, iwapo watapita mtihani wa Atalanta jijini Lisbon.

Mapambano yote ya robo-fainali, nusu-fainali na fainali ya UEFA yatachezewa jijini Lisbon, Ureno.

Mechi zote za robo-fainali zitaanza kupigwa Agosti 12 katika uwanja Jose Alvalade.

Nusu-fainali zitaandaliwa kati ya Agosti 18-19 uwanjani Sport Lisboa Benfica kabla ya uga huo kuwa mwenyeji wa fainali mnamo Agosti 23.

“Madaktari wamelichunguza jeraha la Mbappe na kubaini kwamba aliumia kifundo cha mguu wa kulia na atafanyiwa upasuaji. Atasalia nje kwa majuma matatu,” ikasema sehemu ya taarifa ya PSG.

Mechi dhidi ya St Etienne ilikuwa ya kwanza kwa PSG kusakata tangu kutamatishwa rasmi kwa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Aprili 2020 ambapo PSG walitawazwa mabingwa.

Mbappe aliondolewa uwanjani kwa machela akiwa anatiririkwa na machozi baada ya kukabiliwa visivyo na beki Loic Perrin katika kipindi cha kwanza. Hata hivyo, alirejea uwanjani baadaye kwa usaidizi wa mikongojo na kukalia katika eneo la wachezaji wa akiba wa PSG.

PSG kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Olympique Lyon katika fainali ya French League Cup mnamo Julai 31, 2020, kabla ya kushuka dimbani kupimana ubabe na Atalanta.

Mbappe anajivunia kufungia PSG jumla ya mabao 29 kutokana na mechi 33 za hadi kufikia sasa msimu huu.