Michezo

La Liga yatupa ombi la Granada kutaka mechi yao na Sociedad iahirishwe

November 8th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

GRANADA huenda wakategemea huduma za wanasoka saba pekee wa kikosi cha kwanza kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania itakayowakutanisha na Real Sociedad mnamo Novemba 8, 2020.

Hii ni baada ya ombi lao la kutaka gozi hilo liahirishwe kukataliwa na vinara wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Jumla ya visa 10 vya maambukizi ya Covid-19 vimeripotiwa kambini mwa Granada na wachezaji wote waliosafiri nchini Cyprus kwa minajili ya mechi ya Europa League dhidi ya Omonia Nicosia mnamo Novemba 5, 2020 hawaruhusiwi kuchezea Granada hadi wakamilishe siku 10 za kujitenga. Granada walisajili ushindi wa 2-0 kwenye mechi hiyo ya Europa League ugenini.

Kwa mujibu wa Granada, kuwepo kwa wanasoka saba pekee wa kikosi cha kwanza kambini mwao huenda kukawalazimu kukweza ngazi chipukizi wanne zaidi ambao watakamilisha kikosi chao cha kwanza na pia kuunga timu ya wachezaji wa akiba.

“Kamati ya La Liga inayosimamia ratiba ya mechi imekataa kuahirisha mechi kati ya Granada na Sociedad. Tutasafiri na wanasoka saba pekee hadi San Sebastian kwa minajili ya mchuano huo,” ikasema sehemu ya taarifa ya Granada.

Kwa mujibu wa kanuni za La Liga, mechi haiwezi kuahirishwa iwapo kikosi kina uwezo wa kupanga kikosini idadi ya kutosha ya wanasoka wakiwemo wale wa akiba.

Granada tayari wanakabiliwa na adhabu kutoka kwa La Liga baada ya kusafiri Kwenda Cyprus kushiriki mechi ya Europa League licha ya kuwepo kwa visa vya maambukizi ya corona kambini mwao.