Michezo

Lagat kujaribu kupokonya Kamworor taji la New York City Marathon

August 27th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MWAMERIKA Bernard Lagat ametangaza atajitosa rasmi katika mbio za kilomita 42 wakati wa makala ya 48 ya New York City Marathon hapo Novemba 4, 2018.

Lagat,43, ambaye alibadili uraia kutoka Kenya mwaka 2004, atashindania taji dhidi ya bingwa mtetezi Geoffrey Kamworor na mshindi wa London Marathon mwaka 2017 Daniel Wanjiru kutoka Kenya.

Majina mengine makubwa yaliyothibitisha kuwania ubingwa mwaka 2018 ni mshindi wa Boston Marathon mwaka 2013 na 2015 Lelisa Desisa, na Shura Kitata aliyemaliza London Marathon mwaka 2017 katika nafasi ya pili, wote kutoka Ethiopia, Juan Luis Barrios (Mexico), Waamerika Abdi Abdirahman, Jared Ward na Shadrack Biwott, ambaye ni mzawa wa Kenya aliyebadili uraia, na Mkenya Festus Talam.

Mbio za New York City Marathon huvutia washiriki 50, 000. Pamoja na Tokyo Marathon (Japan), Boston Marathon (Marekani), London Marathon (Uingereza), Chicago (Marekani) na New York City Marathon (Marekani) zinaunda Marathon Kuu Duniani (WMM).