Laikipia: Wabunge wawili ndani

Laikipia: Wabunge wawili ndani

Na WAANDISHI WETU

SERIKALI imechukua hatua kali kurejesha amani katika maeneobunge ya Laikipia Magharibi na Laikipia Kaskazini huku wanasiasa wakinaswa kuhusiana na mapigano hayo.

Waliokamatwa Jumatano ni Mbunge wa Tiaty, William Kamket na aliyekuwa Mbunge wa Laikipia Kaskazini Mathew Lempurkel.

Wawili hao walikamatwa huku hali ya taharuki ikiendelea kugubika eneo la Ol Moran, Laikipia Magharibi kwa siku tisa sasa.

Lempurkel aliyekamatwa katika eneo la Ongata Rongai, Kaunti ya Kajiado, alifikishwa katika Mahakama ya Milimani Nairobi.

Bw Kamket alikamatwa akiwa nyumbani kwake eneo la Kositei, Kaunti ya Baringo, na kisha kupelekwa katika mahakama ya Nakuru chini ya ulinzi mkali.

Alipotolewa kortini, Bw Kamket alipelekwa katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) tawi la Bonde la Ufa mjini Nakuru, na kisha kuhamishiwa kwenye Kituo cha Polisi cha Kaptembwa ambapo alilala usiku kucha.

“Bw Kamket atafunguliwa mashtaka ya kuchochea mapigano katika mahakama ya Nakuru Alhamisi (leo),” akasema Bw Robinson Ndiwa, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Baringo.

Naye Bw Lempurkel alilala katika Kituo cha Polisi cha Kileleshwa jijini Nairobi na anatarajiwa kufikishwa kortini leo ambapo atafunguliwa mashtaka ya uchochezi.

Jumatano, Hakimu Mkazi Sinkiyian Tobiko, alikataa ombi la DCI kutaka Lempurkel azuiliwe kwa siku 14 kuwezesha maafisa wa polisi kukamilisha uchunguzi.

Hakimu alisema maafisa wa DCI wanachunguza makosa yaliyofanyika miezi miwili iliyopita na walifaa kumkamata na kumshtaki mnamo Julai.

Alisema mizozo ya ardhi katika eneo la Laikipia ni ya tangu jadi na hatua ya DCI “kumuamkia Bw Lempurkel na kumtia nguvuni inatiliwa shaka”.

Maafisa wa DCI walisema watamfungulia Bw Lempurkel mashtaka ya mauaji, uharibifu wa mali na uvamizi wa mashamba ya kibinafsi.

Matokeo ya awali ya uchunguzi wa polisi yanaonyesha kuwa, baadhi ya watu wanaoshambulia watu katika eneo la Laikipia ni wafanyakazi wa Bw Kamket.

Juhudi za mawakili kutaka Bw Kamket aachiliwe kwa dhamana katika kituo cha polisi ziliambulia patupu.

Mawakili hao, wakiongozwa na Bw Kipkoech Ngetich walisema kuwa, wanapanga kwenda kortini kutaka serikali kumlipa fidia Kamket kwa kumkamata mara kwa mara kunapotokea mashambulio.

Mshirikishi wa shughuli za serikali kuu kanda ya Bonde la Ufa, George Natembeya jana alionya kuwa serikali itachukua hatua kali dhidi ya wanasiasa wanaochochea wakazi kupinga juhudi za serikali kupambana na majangili wanaohangaisha wakazi wa Laikipia.

“Wanasiasa watakaojaribu kutatiza operesheni ya serikali ya kukabiliana na majangili watachukuliwa hatua kali za kisheria. Wanasiasa wanaenda Laikipia kulia machozi ya mamba, sasa wasikanyage huko,” akasema Bw Natembeya.

Kulingana na Bw Natembeya, wanasiasa wanaochochea mauaji katika eneo la Laikipia watazuiliwa kuwania nyadhifa katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

“Uchunguzi unaonyesha kwamba, mifugo ambao hupelekwa kulishwa katika mashamba ya kibinafsi inamilikiwa na wanasiasa ambao wanafadhili mapigano hayo,” akasema Bw Natembeya.

Alisema wavamizi hao wanalenga kunyakua mashamba hayo ya kibinafsi kwa nguvu na ‘serikali haitaruhusu hilo kufanyika’.

Bw Natembeya alifichua kwamba watu wanane, wakiwemo maafisa watatu wa polisi, tayari wameuawa katika mapigano hayo ndani ya mwezi mmoja.

Lakini Taifa Leo imebaini kwamba idadi ya watu waliouawa katika mapigano hayo ni zaidi ya 10 kwani wale walioangamizwa katika eneo la Ol Moran, hawajajumuishwa kwenye hesabu.

Kulingana na wakazi, dereva wa lori pamoja na taniboi wake ni miongoni mwa waathiriwa waliouawa na majangili hao ndani ya wiki moja.

Kulingana na Bw Benson Muriithi, shahidi, wawili hao walitekwa nyara na majangili na kisha kuuawa Jumatatu.

Ripoti za Richard Munguti, Mercy Koskey, Joseph Openda na Steve Njuguna

You can share this post!

VOLIBOLI: Wafalme Spikers ya Kenya yalipua Misri

Maelfu bado wapigania kuenda Saudia