Laikipia yalipuka

Laikipia yalipuka

Na STEVE NJUGUNA

SERIKALI Jumanne ilipeleka wanajeshi kushirikiana na vitengo vingine vya usalama kwenye operesheni ya kurejesha utulivu katika maeneo yanayokumbwa na mapigano katika Kaunti ya Laikipia.

Hilo lilijiri huku hali ya taharuki ikiendelea kuongezeka katika eneo hilo kwa siku ya saba mfululizo.

Ndege mbili za kijeshi aina ya helikopta zilitumwa kusaidia vikosi vya usalama kwenye operesheni hiyo.

Jumanne, majangili waliojihami vikali walichoma Shule ya Msingi ya Mirigwiti katika eneo la Laikipia Magharibi, ambapo baadaye walifyatuliana risasi na vikosi vya usalama kwa dakika 15. Baadaye, walifanikiwa kutoroka.

Shambulio hilo lilifanyika wakati mshirikishi wa shughuli za Serikali kuu eneo la Bonde la Ufa George Natembeya, alikuwa akizindua operesheni ya kiusalama mjini Ol Moran, umbali wa kilomita nne pekee kutoka shule hiyo.

Kulingana na Bw Natembeya, aliyefika eneo hilo muda mfupi baada ya tukio hilo, majangili hao wanatumia silaha kali hata kuliko polisi wanaoshiriki kwenye operesheni za kuwafurusha.

“Wakati vikosi vyetu vinatumia bunduki aina ya AK47 na G3, majangili hao wanatumia bunduki kali kama M16 na silaha nyingine hatari. Bunduki hizo huwa zinatumiwa na majeshi kutoka nje ya nchi wanapokuja Kenya kushiriki kwenye mafunzo ya kijeshi. Hatujui namna wanavyofanikiwa kupata silaha hizo. Hata hivyo, ni suala linalohitaji uchunguzi,” akasema Bw Natembeya.

Kufikia jana jioni, ndege hizo zilikuwa zikizunguka katika hifadhi ya kibinafsi ya wanyamapori ya Laikipia Nature Conservancy na maeneo yaliyo karibu.

Kulingana na afisa mmoja wa usalama anayefahamu undani wa mikakati inayoendeshwa, jeshi litavisaidia vikosi hivyo kwa ndege ili kuviwezesha kuwanasa majangili wanaohusika kwenye mashambulio katika maeneo hayo.

Alisema uamuzi huo ulifikiwa kwenye mkutano wa Kamati ya Ushauri kuhusu Usalama wa Kitaifa (NSAC) Jumatatu, kama njia ya kuimarisha mikakati ya kukabiliana na wahalifu hao.

Hata hivyo, wanakijiji kutoka sehemu kadhaa katika eneo la Ol Moran, Laikipia Magharibi, waliendelea kutoroka kwa kuhofia mashambulio zaidi kutoka kwa majangili hao.

Kufikia sasa, karibu nyumba 50 zimechomwa katika kijiji cha Kisii Ndogo.

Kando na kutekeleza mauaji, majangili hao wamesababisha uharibifu mkubwa wa mali na mazao.

Kufikia jana, wakazi wengi walikuwa wakitorokea usalama wao kwenye makanisa, vituo vya polisi na maeneo mengine wanayowaona kuwa salama.

“Majangili waliojihami vikali walivamia kijiji chetu Jumamosi na kuchoma nyumba zetu. Walituagiza kuondoka mara moja. Hatuwezi kuendelea kukaa eneo hilo kwa kuhofia maisha yetu,” akasema Bw James Maina, ambaye ni mkazi kwenye mahojiano naTaifa Leo.’

Wakazi waliozungumza na ‘Taifa Leo’ walitaja mashambulio hayo kuwa ya kuogofya na yaliyopangwa.

“Majangili hao huwa wanatekeleza mashambulio hayo nyakati za usiku. Licha ya uwepo wa vikosi vya usalama kutoka vitengo mbalimbali kama vile Polisi wa Akiba na GSU, mashambulio yanaendela kuongezeka. Wametuibia kila kitu na kutuacha pweke,” akasema Bi Mary Wambui, ambaye ni mkazi huku akiwa anabubujikwa na machozi.

Tayari, shule sita zimefungwa kutokana na hali hiyo. Shule hizo ni shule za msingi za Survey, Mirango, Ndunyu Loi, Magadi, Mirigwiti na Shule ya Upili ya Survey.

Viongozi wa eneo hilo, wakiwemo Mwakilishi wa Wanawake Catherine Waruguru na Gavana Ndiritu Muriithi walisema mavamizi hayo kamwe hayahusiani na kiangazi.

Bi Waruguru alisema wakati umewadia kwa Serikali kuchukua hatua kali kwa wakuu wa usalama katika eneo hilo.

You can share this post!

Hisia mseto Zuma akiachiliwa huru kwa msamaha

Wakazi wateketeza lori lililogonga na kuua mwanafunzi