Lalama zazuka baada ya polisi katili kutetewa

Lalama zazuka baada ya polisi katili kutetewa

STELLA CHERONO Na CHARLES LWANGA

Kanda ya video iliyosambazwa mtandaoni ikionyesha polisi wakimshambulia mfanyabiashara wa Naivasha, Bw Frank Koigi na mwanahabari Simon Ben wa runinga ya KBC katika Kaunti ya Nakuru imeongeza visa vya ukatili ambao maafisa hao wanawatendea raia na kutetewa na wakubwa wao.

Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai alisema kwamba kanda iliyosambazwa haikuonyesha kikamilifu kilichotokea na kuonya umma dhidi ya kuwashambulia maafisa wa polisi.

Katika kisa hicho, Bw Koigi ambaye hakuwa na silaha alivamiwa na maafisa watatu wa polisi alipouliza mmoja wao kwa nini alipiga gari lake.

Visa vya polisi kuwatendea ukatili wananchi na kuepuka adhabu vinaonekana kuongezeka kwa sababu ya kulindwa na wakubwa wao.

Mfanyabiashara mwingine katika Kaunti-ndogo ya Malindi, Zackayo Kaibunga anauguza majeraha katika hospitali ya Meridian alikolazwa baada ya kupigwa na maafisa wa usalama.

Bw Kaibunga alivunjika mkono kwenye kisa hicho. Anasema kwamba alikuwa akiendesha gari lake kuelekea nyumbani mwendo wa saa nne na nusu usiku aliposimamishwa na maafisa hao.

Alisema vurugu zilianza alipowasihi polisi wamruhusu aendeshe gari lake hadi kituo cha polisi walipomweleza kwamba walikuwa wamemkamata.

“Walinivuta nje ya gari langu na kuanza kunichapa,” alisema. “Walinitupa ndani ya gari lao na kunipora Sh105,000 nilizokuwa nimetoa benki kuwalipa mishahara wafanyakazi wangu,” aliongeza.

Visa hivi vilivyotokea msimu wa sherehe za Krismasi mwaka huu ni miongoni mwa vingi vya watu kufanyiwa ukatili na polisi licha ya juhudi za mashirika mbalimbali kujitahidi kuhakikisha maafisa wa usalama wanaheshimu haki za binadamu wakitekeleza kazi yao.

Miongoni mwa juhudi hizo ni kubuniwa kwa tume tofauti, kukaguliwa, kuundwa na asasi huru ya kufuatilia utendakazi wa polisi (IPOA), kufanyia mageuzi mfumo na mtaala wa mafunzo ya maafisa wa polisi ili kuhusisha haki za binadamu na kutia nguvu kitengo cha ndani katika idara ya polisi.

Licha ya juhudi hizi, idara ya polisi wa Kenya ina maafisa katili ambao kila siku wanahusika katika ulaji wa hongo na wizi wa mabavu, kudhulumu raia, kuwajeruhi na kuwaua watu wasio na hatia wakidai wanadumisha usalama.

Ndani ya wiki moja, maafisa watano wa polisi wamekamatwa kwa madai ya ulawiti na unajisi na wengine kadhaa wamehusishwa na aina tofauti za uhalifu.

Ingawa maafisa wakuu wanasema kuna mabadiliko, IPOA huwa inalaumu ukatili wa polisi dhidi ya raia. Lakini hatua ya polisi kutetea ukatili wa maafisa hao inawapa nguvu za kuendelea kudhulumu raia wasio na hatia.

Kupitia anwani yake ya Twitter, mwenyekiti wa Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC), Eliud Kinuthia alidai ni Bw Koigi aliyemshambulia afisa wa polisi.

Mnamo Mei mwaka huu, mwanamume na watoto wake wawili walipigwa risasi na maafisa wa polisi wakiwa nyumbani kwao Kibundani, karibu na Ukunda, Kaunti ya Kwale.

Wakati wa kisa hicho, maafisa hao walimpiga risasi mama aliyekuwa mjamzito.Watetezi wa haki za binadamu wanasema kwamba inasikitisha maafisa wa polisi wanawapiga risasi, kuua na kujeruhi watu.

“Inasikitisha kuona maafisa wa polisi wakitendea umma ukatili huu,” asema mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch, Otsieno Nyamwaya.

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Uchaguzi mdogo Nairobi ndio mtihani halisi...

Waislamu waungana kupinga BBI