Michezo

Lampard aitaka Chelsea iwapiku Liverpool na Man City

September 15th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Frank Lampard amewataka masogora wake wa Chelsea kuanza kuwazia kuwa washindani wakuu wa Liverpool na Manchester City katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Hii ni baada ya mwanzo bora wa kikosi hicho katika kampeni za muhula huu ambapo waliwatandika Brighton 3-1 mnamo Septemba 14 uwanjani American Express.

Chelsea walikamilisha kampeni za EPL msimu uliopita wa 2019-20 katika nafasi ya nne japo pengo la alama 33 lilitamalaki kati yao na mabingwa Liverpool waliowanyuka katika mechi zote mbili za ligi.

Katika hatua inayolenga kuanika maazimio ya Chelsea muhula huu, kikosi hicho kwa sasa kimetumia zaidi ya Sh35 bilioni kufikia sasa ili kujisuka upya.

Kati ya sajili wapya waliotegemewa na Chelsea katika gozi dhidi ya Brighton ni mshambuliaji Timo Werner na kiungo Kai Havertz waliosajiliwa kutoka RB Leipzig na Bayer Leverkusen mtawalia.

Ushawishi wa Werner ndio uliohisika zaidi uwanjani na akachangia penalti baada ya kuchezewa visivyo na kipa Mat Ryan. Penalti hiyo ilifumwa wavuni na Jorginho kunako dakika ya 23.

Ingawa alipata jeraha, Werner anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Lampard dhidi ya Liverpool mnamo Septemba 20 uwanjani Stamford Bridge.

Brighton walikabiliwa na pigo la kukosa huduma za sajili mpya Adam Lallana baada ya kupata jeraha kabla ya mwisho wa kipindi cha kwanza. Brighton walisawazishiwa na Leandro Trossard kunako dakika ya 54 baada ya kumwacha hoi kipa Kepa Arrizabalaga anayehusishwa na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea Atletico Madrid au Sevilla nchini Uhispania.

Chelsea walijiweka tena uongozini kupitia kwa Reece James katika dakika ya 56 kabla ya Kourt Zouma kuzamisha chombo cha wenyeji wao dakika 10 baadaye.

Mbali na Werner na Harvertz, Chelsea wamemsajili pia kiungo mvamizi Hakim Ziyech na mabeki Xavier Mbuyamba, Malang Sarr, Ben Chilwell na Thiago Silva msimu huu.

Katika mahojiano yaka na wanahabari mwishoni mwa mechi hiyo, Lampard alifichua kwamba kikosi chake kinakaribia kujinasia huduma za kipa Edouard Mendy kutoka Rennes ili awe kizibo cha Arrizabalaga ambaye kwa sasa ni kipa ghali zaidi duniani.

Ushindi wa Chelsea uliwavunia alama yao ya 2,000 katika EPL baada ya kusakata jumla ya mechi 1,077. Wanakuwa klabu ya tatu kufikia ufanisi huo tangu 1992 baada ya Manchester United (2,234) na Arsenal (2,014).

Tangu mwanzo wa msimu uliopita, Chelsea wamepiga jumla ya mechi 20 za ugenini ambazo sasa zimezalisha mabao 81 ambapo wamefunga 42 nao wakiokota mpira kimiani mara 39.

Klabu hiyo pia imefunga kila mojawapo ya penalti kati ya 16 zilizopita tangu Eden Hazard apoteze mkwaju wake dhidi ya Manchester City mnamo Aprili 2017.

Brighton kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Portsmouth kwenye Carabao Cup mnamo Septemba 17 kabla ya kurejea ligini kuvaana na Newcastle United siku tatu baadaye ugani St James’ Park.